بسم الله الرحمن الرحيم


بسم الله الرحمن الرحيم

UDOMSA.

USHAIRI MZURI

DUNIA YENYE HADAA

Bismillahi naanza kutoa zangu nasaha
wenzangu kuwaeleza yale yenye maslaha
ili kwa Mola muweza tuje kuipata raha
Dunia yenye kupita vipi inatuhadaa.

Kwa nini tuhadaike na maisha ya uongo
waume kwa wanawake tuutulize ubongo
haya yana mwisho wake basi tuyape mgongo
Dunia yenye kupita vipi inatuhadaa.

Rasuli ametwambia tuishi kama wageni
au tunapita njia akhera ndio nyumbani
na sisi hii dunia twaifanya maskani
Dunia yenye kupita vipi inatuhadaa.

Mali na ujana wako ndio hazina za kweli
afya na faragha yako vitumie kwa akili
tumia uhai wako kwa wasia wa rasuli
Dunia yenye kupita vipi inatuhadaa.

Tuishi tunavyopenda tutazikwa kwa hakika
mpende unompenda kaburini hatofika
peke yako utakwenda mwenzio ni amalika
Dunia yenye kupita vipi inatuhadaa.
__________________