بسم الله الرحمن الرحيم


بسم الله الرحمن الرحيم

UDOMSA.

Monday, 20 September 2010

MAONYO NDUGU ZANGU

Assalamu alaykum

Bismillahi Rrahmaani Rrahiim



Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema:

“Nifikishieni ujumbe wangu japo kwa aya moja.”



Uislamu umemharamishia mwanamke kuvaa nguo zenye kudhihirisha na kuonyesha viungo vya ndani vya mwili wake na vile vile zile zenye kubana na kudhihirika umbo lake, khasa zile sehemu zinawavutia watu kama maziwa (matiti), kiuno, matako na kadhalika.



Mambo kama haya ni mabaya sana kwani imesimuliwa katika hadithi sahihi kuwa;

Abu Huraira amesema: Mtume (s.a.w) amesema:

“Watu wa namna mbili katika watu wa motoni sijawaona;

Watu wenye mijeledi (viboko) kama mikia ya ngombe wanawapiga watu (ishara juu ya wale viongozi madhalimu maadui wa watu), na wanawake wavao nguo kama wasiovaa kitu (wako uchi, wanawafundisha wenziwao kufanya kama wao), wakenda hujiringisha na kujikatishakatisha (kiuno, khasa kutikisa matako kwani ndio vutio ya wale wenye maradhi ya uchafu) na vichwa vyao kama nundu za ngamia zilizoinama,hawaingii Peponi wala kusikia harufu yake juu ya kuwa harufu yake itasikika umbali wa masafa kadha wa kadha).”

Hadith



Maelezo ya hadith:

1.Wanawake hawa wametajwa kuwa ni wenye nguo kwa sababu watakuwa wanavaa nguo lakini zisizokuwa na sitara yoyote kwa wepesi wake, na kuonya kwake zikawa zitaonyesha vyote vya ndani kama yalivyo mavazi ya wanawake wetu wa leo wendao uchi (yaani wanavaa nguo lakini kama hawakuvaa), kila kitu kinaonyesha, alama za mavazi ya ndani na kifua wazi, na kusimamisha matiti na kadhalika, na kisha ndio unaambiwa ni dunia ya leo; Dunia ya leo? Basi jiandae na kuwa kuni ya moto wa Jahannam pindi ukijifanya mkaidi na makatazo ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w), na Mwenyezi Mungu atuepushie na moto huo na ndugu zetu wakike wa kiislamu (amin), kwani wao ndio waliotajwa kuwa ndio wengi huko motoni na hii ni pale Mtume (S.A.W) alipokwenda safari ya Miiraj na kuoneshwa hao (wanawake wa umma wake) motoni.



2. Kadhalika vichwa vyao vimesifiwa kuwa ni kama manundu ya ngamia kwa vile namna wanavyoziinua nywele zao na kuzifunga kati ya kichwa, kama kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akipiga mfano wa hawa wanawake wa siku hizi wanaokwenda sehemu maalum kwa ajili ya kunyoshwa nywele zao na kutengenezwa na kufanya mitindo hii na ile, na utakuta wanowatengeneza hivyo ni wanaume (la haula walaanifu wakubwa, tena mabaradhuli) na kazi zote za ulaanisi.



Mtume (s.a.w) amesema:

“Amewalani Mwenyezi Mungu wanawake wanaojifananiza na wanaume, na wanaume wanaojifananiza na wanawake.”

Na hili ni jambo baya sana lililoenea ulimwengu wetu wa kiislamu, khasa huko nyumbani imekuwa ndio mtindo, kwani imefikia hata kuwapo eti maharusi wakioana wanaume kwa wanaume na haya yameshuhudika mwaka juzi huko nyumbani katika moja ya pwani za kitalii nao ati ni Waislamu.

Na pia kuoana wanawake kwa wanawake pia huko nyumbani na haya mambo yanaendelezwa.

Mambo ni khatari sana kwani ni kinyume na maumbile ambayo Mungu amewaumbia, na kinyume na maadili ya Kiislamu, na yanayotufika nyumbani sio kwa sababu ya walio kuwapo madarakani kwa kuwashambulia, lakini ni sisi wenyewe tumewacha mafunzo ya dini yetu, jee leo yasitufike hayo?



Na hawakutosheka na nyumbani, bali yamehamia huko ugenini walipo pia. Hakika habari tunozipata ni za kutisha, watu wavunjiana nyumba kimakusudi kwa kuchukuwa wake za watu, na katika mkasa uliotokea katika moja ya masherehe, wake wa watu wawili kutwangana ngumi mmoja wao akijidai anamchukulia mumewe. (Fa-atabiruu ya ulul absaar).



Mwenyezi Mungu anasema:

“(Na akasema Mtume (akilalamika juu ya kufuru ya qaumu yake); Ewe Mola wangu! bila shaka kuwa qaumu yangu wameihama hii qur-ani.”

Suratul-Furqaan,aya - 30



Maelezo ya aya:

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alimshtakia Mola wake kwa (inadi) ya Makafiri wa Kikuraishi kwa kumpinga na kumpigia mifano ya kila aina. Mara wakimwita Mchawi, Mrogaji, Mwendawazimu, Mshairi n.k, na baada ya kukithiri hayo ndio alirejea kwa Mola wake kumshtakia, (na hatukumuona kuelekea kwa (Kofi Annaan, wala kwa Bush wala kwa Wamarekani walanifu wakubwa maadui wa Kiislamu), na katika aliyoshitaki pamoja na kutokutekelezwa yaliyomo katika maamrisho na makatazo, na pia kuihama kwa kuisoma qur-an!na hii shakwa inahusisha hii qaumu yetu ya kiislamu leo, ni wachache ambao alau wanakumbuka kusoma maneno ya Mola wao wote wameshughulika kutafuta haki zao za kisiasa na mihangaiko ya kidunia yalioambatana na maaasi, bali hufunga misafari ili kwenda kupotosha zaidi waja wa Mungu. Na badala ya kuingia katika miji ya kikafiri na kwenda kuwaelimisha na kuwaongoza katika njia ya istigama, wao ndio wa mwanzo kutoa pesa zao katika maasi na kwenda kuyasherehekea, lau pesa hiyo angaliitolea katika njia ya Mungu ikamfutia madhambi,

Eeh! jamani haki ipo kwa Mwenyezi Mungu.



Leo sikumsikia hata mwanasiasa mmoja kutamka kuwa maadili ya

nchini yamekwenda mrama, lakini tumekuwa tayari kuwapeleka watu katika nchi za kikafir ili wausahau Uislamu, na mengi mingi ambayo hata mengine hayafai kutajwa humu ambayo wanayafanya vijana Wakiislamu wa katika nchi za kikafir, yakiwemo wake kwa waume kuoana na wakristo, kuuza miili yao, kunywa mivinyo, kuvuta mabangi, maherwiin (unga wa cocain) na mengi mengine ambayo yanafuta itikadi na imani ya maadili yao ya Kiislamu.

Kwa hivyo wakubwa zetu msituuze huko!!!!!!!!!!!!!!!.ni wajibu wa kila mtu kuwatanabahisha ndugu zetu wa kiisilamu waliopo uhamishoni katika nchi za kikafiri, juu ya kwenda mrama na mafunzo ya kiisilamu na kuwazindua juu ya mbinu za makafiri za kuwapa hifadhi za kisiasa kwani hawatawacha kujaribu kuwapoteza na kuwatoa katika maadili ya kiisilamu kwa kuwahadaisha kwa anasa za kidunia na kuwabakiza Uisilamu jina bila vitendo.



3. Si haya tu, bali wengi hawaridhiki na nywele zao bali hununua za kubandika.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema:

“Amewalani Mwenyezi Mungu wale wanawake ambao wanaunga nywele zao, na wenye kuwaunga……..”



Hadithi hii inatahadharisha wanawake kutenda hayo ili wasije kosa rehema ya Mwenyezi Mungu. Sasa ikiwa hatuna wivu na ndugu zetu wa Kiislamu wa kike basi yanayotufika hii leo katika misuko suko ya huko nyumbani, mojawapo ni kuwapo viongozi wa dini, lakini hawatimizi wajibu wakutoa maadili ya Kisilamu, watu wameshughulishwa na dunia na siasa tu. Ukimuuliza sharti za sala hajui!, bali hata kutawadha mtu utamkuta anavurumisha tu! hatawadhi sawa sawa.



Sasa ikiwa hali imefikia hivi, basi natusubiri naqama itakayotufika, na yaliyo pita ni zinduo kwa Mwenyezi Mungu jee tutazinduka?



4. Na jambo ambalo ni la kustaajabisha zaidi katika hadithi hii tukufu ni kule kuwekwa pamoja mambo mawili haya ya udhalimu wa kisiasa na uchache wa adabu, kwani mambo haya siku zote yanakuwapo pamoja.



Utaona Madhalimu mara nyingi wanawashughulisha watu wao kwa mambo ya starehe na anasa nyingi, na matamanio ya kibinafsi ili wasahau na kupuuza mambo muhimu yenye maslaha kwa watu wote, kama vile kuhimiza kilimo, elimu bora, afya n.k.



Na turejee kwa Mola wetu na kumuomba huku tukimshtakia kwa hii misuko suko ya dunia inayotufika, kwani yeye ndiye mtarajiwa kwa kila kitu, na pia turejeeni katika kitabu chake ambacho kinatupa kila kitu katika mema, na katika kujikanya na mabaya. Kinyume ya hayo ni sawa na kutia maji ndani ya pakacha.



Ewe Mola tushushie rehema yako kwani sisi waja wako tumejidhulumu kwa kutenda makosa mengi,(Ameen).



Wahenga wanasema:

(Usipoziba ufa utajenga ukuta)



Basi na tuwe tayari kuujenga huo ukuta uliovunjika, na kila mmoja

mkubwa na mdogo washike mpini wa kijengeo.



Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema;

“Kila mmoja ni mchungaji, na kila mmoja ataulizwa kwa anachokichunga.”

Hadith Sahih



WABILLAHI TTAUFIIQ

Thursday, 16 September 2010

SALAM ALAYKUM

NDUGU ZANGU KATIKA IIMANI NAPENDA KUWAKARIBISHA TENA KATIKA MTANDAO HUU WETU. UNAOMILIKIWA NA IDARA YA HABARI NA MAHUSIANAO CHINI YA JUMUIYA YA WANAFUNZI WA KIISLAMU CHUO KIKUU DODOMA (UDOMSA-UNIVERSITY OF DODOMA MUSLIM STUDENTS ASSOCIATION)
TUPO KATIKA NAMNA YA KUBORESHA ZAIDI ILI UJUMBE UWEZE KUWAFIKIA.
PIA TUNAPATIKANA KUPITIA BLOG YETU NYINGINE YAUDOMSA1 nayo PAMOJA NA HII LENGO NI MOJA. ILA KWA SASA TUTATOA UWANJA KWA WANAJUMUIYA NA VIJANA NA MASHEKHE WENGINE KUITUMIA BLOG YETU YA UDOMSA 1 KWA AJILI YA KUTOA NASAHA ZENU KWA UISLAMU WETU NA VIJANA KWA UJUMLA.

Wednesday, 15 September 2010

WATU WEMA WA MFANO.- WANACHUONI WETU

Sheikh Abdullah Saleh Al Farsy

Sheikh Abdullah Saleh Al Farsy
(February 12, 1912 - November 9, 1982)

Mwanachuoni, Mshairi, na Mwana historia maarufu kutoka Zanzibar

Imekusanywa na Muhammad Faraj Salem Al Saiy

Sifa zake

Alipofariki dunia mwaka 1982 Sheikh Abdullah Saleh Al Farsy alikuwa bila shaka yoyote mwanachuoni na mwana historia mkubwa wa Kiislamu na mmojawapo wa washairi wakubwa.
Atakumbukwa daima kwa uso wake mkunjufu usioacha kutabasamu na kwa mwenenedo na tabia zake njema. Wakati wote alikuwa akizungukwa na watu wanaotaka kumsalimia au kupata kutoka kwake mafunzo ya Dini.

Umaarufu wake ulikuwa si katika kisiwa cha Zanzibar na nchi za Afrika ya Mashariki peke yake, bali ulienea hadi Somalia ya kusini na ya kaskazini, Cape Town upande wa kusini mpaka kufikia Malawi, mwahali alipokuwa akitoa darsi zake kabla ya kuhamia Kenya kwa kuhofia kukamatwa na serikali ya Zanzibar.

Alizaliwa Zanzibar mwezi wa February mwaka 1912 katika ukoo maarufu, akajifunza Qur-aan kutoka kwa Fatma Hamid Said (1854-1936), aliyesoma kwa Sheikh Amin bin Ahmed aliyekuwa akifundisha Qur-aan kijiji cha Jongeani mahali alipozaliwa Sheikh Abdullah Farsy na kukulia.

Sheikh Abdullah Saleh Farsy alihifadhi Qur-aan yote pamoja na hadithi nyingi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) akiwa na umri mdogo sana, na shauku yake kubwa isiyotoshelezeka ya kujifunza masomo ya Kiislamu na ya kiulimwengu ilionekana pale wenzake walipokuwa wakijishughulisha na michezo na anasa za kidunia, wakati yeye alikuwa kila siku akizama katika kusoma kitabu kipya cha mafunzo ya Kiislamu.
Alikuwa akipenda sana kusoma kiasi ambapo maisha yake yote yalifungika ndani ya maktaba 'library' yake kubwa ya nyumbani.

Alipofariki dunia, Sheikh Abdullah Saleh al-Farsy alikuwa Aalim mwenye kutambulika na kuheshimika kupita wote katika nchi zinazotumia lugha ya Kiswahili. Mchango wake usiokuwa na mfano katika kuelimisha watu dini ya Kiislamu ulifikia kiwango chake cha juu baada ya kuchapicha tafsiri kamili ya mwanzo ya Qur-aan Takatifu ya Kiswahili iliyokubaliwa rasmi yenye kurasa 807.

Elimu yake

Alipokuwa kijana, mwanachuoni huyu mwenye hamasa na uhodari alibahatika wakati ule kuwepo na kuenea kwa vyuo vikongwe vya Kiislamu vilivyojaa wanafunzi chini ya uongozi wa Maulamaa weledi mfano wa Sheikh Abu Bakar bin Abdullah bin Bakathir (1881-1943) aliyekuwa mwanafunzi maarufu wa Sayyid Ahmed bin Abu Bakar al-Sumait (1961-1925)

Katika mwaka wa 1922 Sheikh Abdullah Saleh Farsy alijiunga na chuo cha Msikiti Barza baada ya Maulamaa wawili kumtaka afanya hivyo:
Wa kwanza alikuwa Sayyid Hamid bin Mansab (1902-1965) aliyemfunza RISALATUL JAMI'A, yenye mafunzo ya taasisi ya Kiislamu. Imamu huyu wa msikiti wa Forodhani aliyefariki dunia wakati akitoa darsi ndani ya msikiti Gofu alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Muhammad Abdul Rahman Makhzymy (1877-1946), mmojawapo wa waalimu wa Sheikh Abdullah Saleh Farsy.
Wa pili alikuwa Sayyid Alawy bin Abdul Wahab (1902-1960) aliyemsomesha vitabu 12 vya Fiq'hi katika lugha ya kiarabu pamoja na sharhi ya MARDFIN RABBIYYAH juu ya elimu ya urithi.

Baada ya kuwa mjuzi katika elimu ya taasisi ya Kiislamu katika chuo cha Msikiti Barza, Sheikh Abdullah Saleh Farsy alikuwa mjuzi pia wa elimu ya nahau ya lugha ya Kiarabu. Na alipokuwa na umri wa miaka 20 alikuwa akiandika mashairi ya Kiarabu, dalili ya daraja kubwa ya elimu ambayo Maulamaa wa Zanzibar wakati ule waliweza kuieneza.

Sheikh Abdullah Saleh Farsy alijifunza chini ya Maulamaa wengi wakubwa kama vile Sheikh Ahmed bin Muhammad al-Mlomry (1873-1936) aliyemfundisha vitabu 25 vikiwemo Tafsiri ya Jalalayn kilichoandikwa na Jalal al-Din Mahali (1389-1450) kutoka Misri na Jalal al-Din Suyuti (1445-1505), Syria, na hawa ni Maulamaa wakubwa na maarufu wa madhehebu ya Imam Shafi.

Baada ya kuhitimu darsi zote katika chuo cha Msikiti Barza, Sheikh Abdullah Saleh Farsy aliruhusiwa na Sheikh Ahmed bin Muhammad al-Mlomry kusomesha katika chuo hicho katika mwezi wa Ramadhan chini ya uangalizi wake.

Alijifunza pia kutoka kwa Sheikh Abu Bakar (1881-1943), mtoto wa Sheikh Abdullah bin Abu Bakar Bakathir (1860-1925), mwanafunzi wa Sheikh Ahmed bin Abu Bakar al-Sumait.
Sheikh Abu Bakar bin Abdullah bin Bakathir aliyejifunza kutoka kwake elimu ya Fiq'hi kupita Maulamaa wengi hapo Zanzibar, alikuwa akihudhuria darsi za Sheikh Abdullah Saleh Farsy kwa ajili ya kumpa moyo, kisha akamchagua kuwa Imamu wa Swalah ya Witri kutoka mwaka 1933 mpaka terehe 28 October 1939, alipomruhusu pia kusoma Qur-aan katika Msikiti Gofu na hatimaye akawa anasalisha Swalah ya Alfajiri mpaka mwaka 1966 alipochukuwa mahali pake mtoto wa dada yake Saleh bin Salim bin Zagar.

Sheikh Abdullah Saleh Farsy alisoma vitabu vingi vya Fiq'hi kutoka kwa Sheikh Muhammad Abdul Rahman al-Makhzymy vikiwemo vitabu vya Fathul Muin na Iqnai, ambavyo mwanzo vilikuwa vikisomeshwa na Sheikh Abdullah bin Abu Bakar bin Bakathir hapo Msikiti Gofu katika mwaka 1917.
Alijifunza kutoka kwake pia elimu ya kupanga nyakati za Swalah na kuujua upande wa Qiblah.

Juu ya kuwa hapo mwanzo Sheikh Abdullah Saleh alisoma Minhaaj At Tabiiyn kitabu cha Sheikh Zakariya Muhyddin Yahya Sharaff ad-Din al-Nawawi (1213-1277) ambaye ni mwanachuoni mkubwa wa madhehebu ya Kishafi, lakini baadaye alisoma tena kitabu hicho kwa Sheikh Muhammad Abdul Rahman al-Makhzymy.
Msimamo wa kisheria wa kitabu hiki hapo Zanzibar umeanzia zama za Imam Abu Hamid bin Muhammad al-Ghazzali (1058-1111), aliyekuwa mwanafunzi wa Imam wa Haramayn Ahmed Malik al-Jawayti (1085) kutoka kwa Ayoub al-Buwati (845), mwanafunzi wa Imam Muhammad Idriys al-Shafi'i (767-820), mwanzilishi wa Madrasa ya Shafi'i, yenye wafuasi wengi Zanzibar na Misri.

Sheikh Muhsin bin Ali bin Issa Barwan aliyekuwa mwalimu wake Msikiti Gofu, alikuwa mwanachuoni wa mwanzo katika mwaka 1944 kumruhusu Sheikh Abdullah Saleh Farsy kusomesha Jalalayn Msikiti Barza katika mwezi wa Ramadhani. Baadaye Sheikh Abdullah Saleh Farsy alijifunza kwa Sheikh al-Amin Ali bin Abdullah bin Nafi al-Mazrui mwaka (1875-1947), aliyeupendezesha kwa watu Uislamu wa kisasa kama ulivyoshereheshwa na Shekh Muhammad Abduh (1845-1905), aliyemsomesha Sheikh Ahmed Muhammad Mlomry katika chuo kikuu cha al Azhar, Misri.
Sheikh Abdullah Saleh Farsy alipewa Ijaza (shahada) na Sheikh ‘Umar bin Ahmad bin Abu Bakar al-Sumait (1896) aliyemsomesha vitabu vya Fiq'hi, Mantiq (Logic) na Hadith, pamoja na vitabu vingine. Bahati mbaya mwanachuoni huyu alirudi Yemen katika mwaka wa 1965 kutokana na udikteta uliokuwepo Zanzibar chini ya serikali iliyoongozwa na mkiristo Julius Kambarage Nyerere.

Umahiri aliouonyesha Sheikh Abdullah Saleh Farsy katika elimu ya mambo ya kidunia ulikuwa mkubwa pia. Alikuwa hodari sana katika elimu hiyo, na alipokuwa Central Primary School aliyojiunga nayo mwaka 1924, mwalimu wa lugha ya Kiingereza alishindwa kuamua darasa lipi ampeleke. Sheikh Abdullah Saleh Farsy aliyemaliza miaka minane inayotakiwa katika shule ya msingi katika muda wa miaka mitano tu.
Miongoni mwa walimu wake maarufu alikuwa Sheikh Abdullah bin Ahmed bin Seif (1900-1940) na Sheikh Abdul Bary kutoka chuo kikuu cha Al-Azhar aliyeajiriwa na Sayyid Ali bin Humoud mwaka (1902-1911).

Qur-aan Takatiku

Aliandika tafsiri yake ya Qur-aan Takatifu kuanzia mwaka wa 1950 hadi mwaka 1967, wakati fikra za umoja wa Kiislamu na Uislamu wa kisasa ulipokuwa ukifanyiwa kampeni kubwa hapo Zanzibar.
Wakati huo huo Tafsiri hii ilikuwa ni jibu la tafsiri ya Qur-aan Tukufu aliyoiandika Padri Godfrey Dale kwa ajili ya kuwawepesishia wahubiri wa Kiafrika walioajiriwa na University Mission to Central Africa (UMCA), iliyoanzishwa mwaka 1873 na Padri Dr. David Livingston (1813-1873) huko Zanzibar.
Tafsiri ya Padri Dale iliyoandikwa kwa Kiswahili cha Kiunguja ilikuwa na kurasa 542 pamoja na kurasa 142 za sharhi, ilipigwa chapa mwaka 1923 huko London na jumuiya ya kueneza elimu ya Kikristo (Society for Promoting Christian Knowledge).
Kwa vile tafsiri hiyo iliandikwa kwa njia ya kuutetea Ukristo, jambo lisilokubalika kwa Waislamu, Sheikh Mubarak bin Ahmed bin Ahmad, mkuu wa Makadiani Afrika Mashariki (Ahmadiyah Muslim in East Africa) aliamua kuanza kuandika tafsiri yake mwaka 1936 iliyokubaliwa na kutambuliwa na wamisionari hapo Zanzibar.
Katika mwaka 1942 nakala ya tafsiri ya Makadiani iliyopigwa taipu ilipelekwa mbele ya kamati ya lugha ya Kiswahili   (Inter-Territorial (Swahili) Language) kwa ajili ya kukubaliwa rasmi kilugha. Na katika mwezi wa April mwaka 1944, kamati ilijibu kwa kuikubali lugha iliyotumika ikitaka baadhi ya marekebisho kufanyika. Juu ya kuwa masahihisho yote hayakufanyika kama ilivyotakiwa, tafsiri hiyo ikapelekwa mbele ya baadhi ya viongozi wa Makadiani wa Afrika ya Mashariki na kukubaliwa kuwa lugha iliyotumika ni nzuri na yenye kukubalika.

Sheikh Amri bin Abeid (1924-1964), aliyejifunza Ukadiani huko Pakistan mwaka (1954-1956) alijaribu kuitetea tafsiri ya Makadiani, lakini tafsiri hiyo iliyopigwa chapa kwa mara ya mwanzo mwaka 1953 ilisababisha mgogoro mkubwa kutoka kwa Masunni waliowatuhumu Makadiani kuwa wamebadilisha na kugeuza baadhi ya maneno kwa kusudi la kuunga mkono fikra zao.
Ili kupambana na tafsiri za Wakristo na Makadiani zilizogeuzwa na kubadilishwa ilionekana kuwepo umuhimu na dharura ya kupatikana tafsiri yenye kutambuliwa rasmi. Jukumu hilo akabebeshwa Sheikh Abdullah Saleh Farsy, aliyekuwa akimuomba Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu asife kabla ya kuikamilisha tafsiri hiyo.

Fikra hii adhimu ilianza baada ya Sheikh kupiga chapa kitabu chake cha mwanzo kiitwacho 'Maisha ya Mtume Muhammad' (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) kilichofuatiliwa na kitabu cha Sura za Swalah na Tafsiri zake mwaka (1950).
Kabla ya kudhihirisha kutoridhika kwake na tafsiri ya Makadiani katika kijitabu kidogo ‘Upotofu wa Tafsiri ya Makadiani’, Sheikh Abdullah Saleh alikwishawahi kuandika tafsiri na sharhi ya Surah Yaseen, Al-Waqiah na Al- Mulk kilichopigwa chapa na A.A. Vasingstake, Uingereza na kutolewa mwaka 1950 Zanzibar.
Tafsiri yake aliyoiandika kwa kuitegemea zaidi tafsiri ya Jalalayn ilianza kupigwa chapa juzuu baada ya juzuu, na baina ya mwaka 1956 na 1961 juzuu kumi na mbili zilikwishapigwa chapa.
Kutokana na upungufu wa fedha, tafsiri iliyokamilika ilipigwa chapa mwaka 1969 na wadhamini walikuwa The Islamic Foundation.
Msaada mkubwa uliotolewa na Sultani wa Qatar, Sheikh Ahmad bin Ali uliwezesha kugawiwa bure misahafu 4,000 na kuuzwa misahafu mingine 3,000 kwa bei nafuu ya shilingi kumi tu.

Kuanzia mwaka 1950 hadi 1960 kampeni kubwa dhidi ya Makadiani ilifanywa na Jamaat al Islam huko Pakistan chini ya uongozi wa Sheikh Maududi (1903-1979) aliyezikaribisha juhudi kubwa za Sheikh Abdullah Saleh Farsy, juu ya khitilafu iliyokuwepo baina ya misimamo ya Zanzibar na Pakistani, kwani Sheikh Abdullah Saleh Farsy hakuwa akiona tofauti yoyote baina ya Makadiani na Ahmadiya waliojitenga na Makadiyani. (Ahmadiya ni kundi lililojitenga na Makadiani kutokana na baadhi ya khitilafu baina yao)
Islamic Foundation ya Nairobi yenye kuunga mkono Jamaat al Islam ya Pakistan, ndiyo iliyopiga chapa kwa mara ya mwanzo Tafsiri ya Sheikh Abdullah Saleh Farsy, aliyeandika kuwa Maududi ameikubali tafsiri yake ya QURANI TAKATIFU. Na Sheikh Abdullah Saleh Farsy naye alieleza kuikubali kwake tafsiri ya Maududi inayoitwa 'Qur'an Fahmi Ke Bunyadi Usul' (Msingi wa kuifahamu Qur-aan), na akaruhusu uandikwa utangulizi wa Tafhim Al-Qur-aan katika Qurani Takatifu.

Mafundisho yake

Kuanzia tarehe 7 Januari 1960 hadi 19 Februari 1960 Sheikh Farsy alikuwa safarini Nyasaland 'Malawi' na Rhodesia ya Kusini akitoa darsa na kuwahutubia Waislamu na kuwanasihi juu ya umuhimu wa kujifunza masomo ya dini.
Tarehe 11 April 1960 baada ya kurudi kutoka Nyasaland, Sheikh Farsy aliandika ripoti aliyoeleza ndani yake umuhimu wa mafunzo ya dini. Aliwataka wanaohusika kutilia nguvu umuhimu wa kuwapatia Waislamu elimu katika skuli za serikali.
Aliandika: "Kwanza, upeo wa elimu ya watoto wa Kiislamu ni duni ukilinganisha na wasiokuwa Waislamu katika Nyasaland. Kuwepo kwa jamii mbili katika nchi, mojawapo imeelimka na nyengine haijaelimika ni hatari kwa serikali na kwa jamii. Serikali ni baba wa wananchi wote, na kwa ajili hiyo inapaswa kutopendelea upande mmoja."
Aliendelea kueleza: "Serikali inatoa misaada mbali mbali kuipa skuli za wamishionari bila ya kuzilamisha kujiunga na skuli za serikali. Jukumu la serikali ya Nyasaland lazima liwe kuinyanyua daraja ya elimu kwa Waisalmu iwe sawa na ile ya jamii nyingine nchini.”

Matakwa ya Sheikh Farsy juu ya kuelimishwa Waislamu hayakuwa kutaka wajengewe skuli zao tu, bali yalikuwa makubwa kuliko hivyo. Alitilia mkazo jambo la kuajiriwa waalimu wa dini ya Kiislamu katika skuli za serikali pia. Alisema: "Shule za serikali hazina budi kuwa na walimu watakaosomesha mafunzo ya Kiislamu wenye kulipwa na serikali. Inashangaza kuona kuwa waalimu wa Kikristo katika shule hizo wanalipwa na serikali wakati waalimu wa Kiislamu wanalipwa na jamii. Haya hayafahamiki."

Kupitia darsi zake za misikitini na kwa njia ya vitabu, Sheikh Farsy alitumia juhudi zake zote katika kuwaelimisha vijana misingi asili ya Kiislamu. Alihimiza na kutilia nguvu umuhimu wa kufufua, kufuata na kuyafahamu mafundisho sahihi ya dini kama yalivyokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) na Sahaba zake (Radhiya Llahu anhum) pamoja na mafundisho ya watu wema waliotangulia 'Salafus Swaalih'.
Mafundisho haya yalikuwa yakifundishwa kabla yake na Sheikh Al-Amin na Sheikh Muhammad Kassim hapo Mombasa.
Lengo la Sheikh Farsy lilikuwa kubwa kupita wadhifa wake wa Kadhi mkuu wa Kenya.  Lengo lake lilikuwa ni kupata jukwaa litakalomwezesha kuifufua na kuieneza elimu sahihi ya dini kama ilivyokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam), na kuwakataza watu kufuata uzushi ‘bid’aah’ na itikadi zisizo na misingi ya Kiislamu, na mambo yaliyo batili ambayo hao wanaoyaeneza wanajaribu kuyanasibisha na Uislamu.                

Sheikh Farsy alifanikiwa kiasi kikubwa sana, na watu wengi waliokuwa wakihudhuria darsa zake walikuwa wakihisi kuwa mafunzo yake yanaingia moja kwa moja ndani ya nyoyo zao. Kwa juhudi zake, alifanikiwa kuanzisha kizazi kilichoiendeleza kazi yake hiyo ya kupiga vita uzushi na ushirikina, na kufanikiwa kuondoa itikadi nyingi ambazo watu wakati huo walikuwa wakidhani kuwa yamo katika dini.

Safari zake

Baada ya kukamilisha masosmo yake katika Chuo cha Ualimu 'Teachers Training College (TTC)', Sheikh Abdullah alisomesha shule za msingi kuanzia mwaka 1932 hadi 1947, na kutokana na jitihada zake kubwa katika kazi, alipewa cheo cha Mkaguzi mkuu wa shule za msingi za Unguja na Pemba kuanzia mwaka 1949 hadi mwaka 1952. Kisha akapewa cheo cha Principal wa Muslim Academy Secondary School kuanzia mwaka 1952 hadi 1956 kabla ya kuchaguliwa kuwa  Mwalimu mkuu 'Headmaster' wa Arabic Medium School kuanzia mwaka 1957 hadi 1960.

Mwezi wa Machi mwaka 1960, Sheikh alikwenda kuhiji na katika mwaka wa 1967 alijiuzulu kazi katika Wizara ya Elimu alipokuwa mwalimu katika Chuo cha Ualimu 'Teachers' Training College.

Katika mwaka 1960, alichaguliwa kuwa Kadhi mkuu wa Zanzibar, na aliendelea na kazi hiyo muda wa miaka saba, mpaka alipoamua kuiacha na kuhamia Kenya baada ya mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliyosababisha umwagaji mwingi wa damu huko Zanzibar pamoja na kukamatwa na kutiwa ndani bila sababu kwa viongozi wengi wa kisiasa na wa kidini.

Mwenyeji wake huko Kenya alikuwa Sheikh Muhammad Kassim al-Mazrui, sahibu yake wa zamani tokea waliposoma pamoja chini ya mwalimu wao Sheikh al-Amin bin Ali al-Mazrui, aliyekuwa akifundisha dini huko Zanzibar.

Sheikh Abdullah Saleh Farsy hakuwa mgeni huko Kenya ambako sifa zake kuwa mwanachuoni mkubwa zilitangulia kufika kabla yake. Sheikh Muhammad Kassim al-Mazrui ndiye aliyempendekeza kwa Rais Jomo Kenyatta kupewa cheo cha Kadhi mkuu wa Kenya, jambo ambalo Rais Kenyatta alilikubali bila kipingamizi.
Kwa muda wa miaka 14 alikuwa Kadhi mkuu wa Kenya, daraja yenye heshima kubwa sana aliyoitumikia kwa muda wote huo kwa ikhlasi, hekima, uwezo wa hali ya juu, na uerevu mkubwa sana mpaka alipoamua kustaafu katika mwaka 1980.

Kifo chake

Sheikh Abdullah Saleh Farsy alifariki dunia tarehe 9 Novemba mwaka 1982 karibu miezi minane tokea alipoondoka Kenya kuelekea Muscat - Oman kwa ajili ya kuungana na aila yake.

Huzuni kubwa iliyoingia nyoyoni mwa Waislamu wa Afrika Mashariki kutokana na kifo chake itaendelea muda mrefu sana, na pengo lake kamwe si rahisi kuzibika, na watu wataendelea kufaidika na elimu aliyowarithisha daima milele.


Wadhifa zake

·        Mwalimu – Shule za msingi (1932 - 1947)
·        Mkaguzi mkuu  wa Shule za Msingi - Zanzibar na Pemba (1949 - 1952)
·        Principal - Muslim Academy Secondary School (1952 - 1956)
·        Mwalimu mkuu - Arabic Medium School (1957 - 1960)
·        Kadhi mkuu wa Zanzibar (1960 - 1967)
·        Mwalimu - Teacher Training College (? - 1967)
·        Kadhi mkuu wa Kenya    (1974 - 1980)

Darsi zake

Alipokuwa Mombasa, Kenya Sheikh Farsy alikuwa akitoa darsa zake katika misikiti ifuatayo:
·        Msikiti Sakina (Majengo)  kila Jumanne
·        Msikiti Al-Azhar (Guraya)  kila Al Khamisi
·        Msikiti Shihab (Mwembe Tayari) kila Jumatano
·        Msikiti Mlango wa papa (mji wa Kale) Jumatatu
·        Msikiti Ridhwaan (King’orani) Ijumaa
·        Msikiti Muhammad Rashid (Kaloleni Mazui) Jumatatu-mara moja kila mwezi
·        Tunah (Majengo) Ijumaa moja
·        Msikiti Nur (Ijumaa moja)
·        Malindi, Kenya
·        Msikiti Sheikh Nassor. (Jumamosi baada ya Swala ya Magharibi)

Vitabu vyake:

·        Tafsiri ya Qurani Takatifu.  Ilipigwa chapa mara ya mwanzo mwaka 1969
·        Maisha ya Nabii Muhammad
·        Mawaidha ya Dini
·        Tarehe ya Imam Shafi na Wanazuoni wakubwa wa Afrika ya Mashariki
·        Baadhi ya Wanachuoni wa Kishafi wa Mashariki ya Afrika.
·        Sayyid Said bin Sultan
·        Urathi
·        Jawabu za Masuala ya dini (sehemu ya kwanza, pili na tatu)
·        Tafsiri ya Suratul Kahf na hukumu ya swala ya Ijumaa
·        Sura za swala na tafisir zake
·        Swala na maamrisho yake
·        Ndoa na maamrisho yake
·        Saumu na maamrisho yake
·        Mambo anayofanyiwa Maiti na Bidaa za Matanga na hukumu za Eda
·        Bidaa I na II 
·        Khitilafu za Madhehebu Nne katika swala
·        Sifa za Mtume, mawaidha na Dua
·        Mashairi I-II
·        Maisha ya Sayyidnal Hassan
·        Maisha ya Sayyidnal Hussein
·        Utukufu wa swala na namna ya kusali
·        Mafunzo ya dini
·        Tafsiri ya Maulidi Barzanji neno kwa neno
·        Wakeze Mtume wakubwa na wanawe wengine
·        Wakeze Mtume wadogo
·        Tafsiri ya Baadhi ya Sura za Qurani: Yasin, Waqia na Mulk Sayyidna Khalid bin Al-Walid
·        Vyakula alivokula Mtume
·        Tunda la Quran
·        Upotofu juu ya Tafsiri ya Makadiani
·        Kisa cha Miraji
·        Maisha Ya Mtume Muhammad

Vitabu vya Kiarabu:
·        Al-Busa’idiyyun hukkam Zinjibar. Muscat: Ministry of National Heritage and Culture 1982.

Vitabu vyake visivyopigwa chapa: (kiarabu)
·        1. Inayatullaahi al-adhym bi al  Qurani al-Karim
·        2. Irfaani al ihsaan bi tarjamati al qarii Hafs bin Suleiman
·        3. Nuru al basira wal al basar fi taraajimi al quraa al arba’atashar
·        4. Al khulafau al Amawiyin [28]

ELIMU YA KURAN-ULUMU L QUR – AN


ULUMU L QUR – AN
Ulumul Qur – an, maana yake ni ‘Elimu inayohusiana na Qurani’, na elimu yenyewe sio ya tafsiri ya Qurani, bali ni elimu inayohusiana na kuijuwa Qurani, maana yake, vipi imeshuka, aya gani zilizotangulia na zipi zilizoteremshwa baadaye, sura ipi Iliyoteremshwa Makka na ipi ya Madina, aya ipi iliyofutwa na ipi iliyofuta, vipi imekusanywa na kuandikwa na mambo mengi mengine.
Imam Shafi (Rahimahu llah) alipoletwa mbele ya Khalifa wa Waislam Harun Al Rashid baada ya kusingiziwa uongo na Amiri aliyekuwa akitawala wakati huo huko Yemen, aliletwa akiwa amefungwa minyororo hadi shingoni pake.
Baada ya kuulizwa masuali mengi na Khalifa huyo akamtaka aelezee nini anachojuwa kuhusu Elimu ya Qurani.
Imam Shafi akajibu;
“Hakika Elimu za Qurani ni nyingi, je! Unaniuliza juu ya aya zisizobeba isipokuwa maana moja tu (Muhkam) au zinazobeba maana zaidi ya moja (Mutashabih) au ipi iliyotangulia na ipi iliyokuja baada yake (Taqdiym na Taakhiyr) au unataka kujuwa ipi iliyofutwa na ipi iliyofuta (Nasikh na Mansukh) au juu ya ………?”
Akaendelea hivyo huku akijibu kila suala analoulizwa na Harun AL Rashiyd mpaka Khalifa huyo akahakikisha kuwa huyu ni Alim wa kweli, akaamua afunguliwe na kupewa heshima zote wanazopewa Maulamaa.
MFANO WA AYA ZILIZOFUTA NA ZILIZOFUTWA (NASIKH NA MANSUKH)
Mwenyezi Mungu anasema;
“Aya yo yote tunayoifuta au kuisahahuliza tunaleta iliyo bora kuliko hiyo au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu?”.
Al Baqarah- 106
Imam AL Shafi-i (Rahimahullah) anasema;
“Mwenyezi Mungu hafuti hukmu isipokuwa ataleta badala yake hukmu nyingine. Mfano pale alipoifuta hukmu ya kuelekea Baytul Maqdis katika Sala na akaileta badala yake hukmu ya kuelekea Al Kaaba”.
Imam Shafi akiendelea kutoa mifano alisema;
“Mwenyezi Mungu anasema;
“Ewe Mtume (wa Mwenyezi Mungu)! Wahimize walioamini wende vitani. Wakipatikana kwenu watu ishirini wanaousubiri watashinda mia mbili (katika hao makafiri. Basi nyinyi mkiwa ishirini lazima msimame mupigane na watu miteni).
Na kama wakiwa watu mia moja kwenu watashinda elfu moja ya wale waliokufuru, maana hao ni watu wasofahamu. (Basi watu mia katika nyinyi wasiwakimbie watu elfu katika wao)”
AL Anfal – 65
Katika aya hii Mwenyezi Mungu anatujulisha kuwa Waisalm wanazo nguvu za Imani kiasi ambapo Waislam ishirini wanaweza kupigana na makafiri mia mbili na kwamba Mwislam mmoja anatakiwa asikimbie akipambana na makafiri kumi.
Lakini baada ya Mwenyezi Mungu kuona kuwa upo udhaifu, na hii inatokana na vita kuendelea mda mrefu, Mwenyezi Mungu akapunguza pia idadi, kwa kutujulisha kuwa sasa Waislam mia moja wanaweza kuwashinda makafiri mia mbili. Muislam mmoja anatakiwa asikimbie akipigana na makafiri wawili.
Mwenyezi Mungu anasema;
“Sasa Mwenyezi Mungu amekukhafifishieni maana anajua ya kwamba kuna udhaifu (sasa) kwenu (kwa kuwa vita vimeendelea kwa mda mrefu). Kwa hivyo wakiwa watu mia moja kwenu wenye subira na wawashinde watu mia mbili kwao; na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu nawawashinde elfu mbili; kwa amri yaMwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri (yaani sasa wanaambiwa kila Muislam mmoja akabiliane na makafiri wawili)”.
AL Anfal – 66
Hii ni mifano miwili katika kuisherehesha maana ya kufutwa aya na kuletwa nyingine badala yake, na tumeona kuwa; Aya yoyote inapofutwa haina maana kuwa haisomwi tena, bali inasomwa kama Aya nyingine isipokuwa hukmu yake hubadilishwa kwa hukmu nyingine.
Ingawaje Elimu za Qurani ni nyingi na zina mpangilio wake maalum wa kuandikwa, lakini leo sitoanza kwa mpangilio huo na badala yake nitazungumza moja kwa moja juu ya jambo linalotohusu zaidi kwa wakati huu, nalo ni;
Kuteremshwa Qurani kwa herufi saba na jinsi ilivyoandikwa na kukusanywa wakati wa Mtume(SAW) na jinsi ilivyokusanywa wakati wa Abubakar(RA) na hatimaye wakati wa Othman(RA)”.
Kabla ya yote ningependa tutambue kuwa Itikadi yetu ni kuwa; Hatuamini kuwa kulikuwa na aya yoyote au hata herufi moja iliyoondolewa kutoka katika Qurani, bali tunaamini kuwa msahafu huu tunaousoma sasa na yale yaliyomo ndani yake ni yale yale yaliyokuwemo tokea wakati wa Mtume(SAW) alipokuwa akiishi na akiteremshiwa Wahyi.
Isipokuwa pana tofauti ya misomo (Qira aat) na pia pana hadithi mbili zinazowababaisha baadhi ya watu na kufikiria kuwa kulikuwa na Aya mbili ndani ya Qurani na kwamba sasa hazipo tena. Aya hizi zinajulikana kama ifuatavyo;
a- Ayatul Rajm
b- Ayatul Ridha a.
Baadhi ya watu walidhania kuwa hizi ni Aya na kwamba zilikuwemo ndani ya Qurani, na Inshaallah kila tunapoendelea mbele na darsi hii tutatambua ukweli kuwa hizo si Aya na wala hazikuwemo ndani ya Qurani.
KUTEREMSHWA QURANI KWA MISOMO SABA
Mtume(SAW) aliteremshiwa Qurani kwa misomo saba. Hadithi nyingi zilizo sahihi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume(SAW), zinasema kuwa Jibril(AS) alimsomesha Mtume(SAW) Qurani kwa msomo wa aina moja, kwa lugha ya ki Qureshi, lakini Mtume(SAW) alimtaka Jibril(AS) amuombe Mwenyezi Mungu iongezwe misomo mingi zaidi kwa sababu wakati ule Waislam wepya walikuwa wengi na wangepata taabu sana kuifaham Qurani kwa msomo wa lugha moja ya ki Qureshi peke yake, hasa kwa vile walikuwa wapo watu wa tabaka mbali mbali, makabila mbali mbali na kutoka mataifa mbali mbali.
Mtume(SAW) anasema;
“Jibril alinisomea Qurani kwa herufi (msomo wa aina) moja, nikamwambia aniongezee mpaka ikafikia misomo saba”
Bukhari na Muslim
Waarabu katika lugha yao wana misemo mbali mbali, isipokuwa lugha ya ki Qureshi ndiyo iliyokuwa ikitumika zaidi, na ndiyo iliyoandikiwa Qurani, na hii inatokana na kuwa wao ndio walinzi wa Nyumba kongwe (Al Kaaba), na wao ndio waliokuwa wakiwahudumia Mahujaji hata kabla ya kuja Uisalmu.
Katika lugha ya Kiswahili kwa mfano, utakuta misemo ya aina mbali mbali, ikibeba maana moja.
Tanzania bara utakuta herufi R inatamkwa L na herufi L inatamkwa R. ‘Nyanya’ inaitwa ‘tungule’ na tungule inaitwa ‘nyanya’.
Ama Kenya, neno ‘njoo’ wanasema ‘ndoo’ na katika kiswahili cha Tanzania neno ‘ndoo’ ni ile inayotekewa maji. Bali wakati mwingine utakuta neno kamili hubadilika kwa mfano neno ‘kuhama’ kule Kenya wanaita ‘kugura’.
Na hivi ndivyo ilivyo katika lugha ya kiarabu, kwa mfano neno mpira huitwa ‘Kurra’ lakini ukenda Yemen katika mji wa Aden, mpira unaitwa ‘kubba’ na sio ‘kurra’, na ukiondoka hapo Aden na kuelekea Hadhramout utaona kuwa neno ‘kubba’ maana yake ‘kaburi’.
Na Masri pia kuna matatizo yake, hasa katika kuitamka herufi ‘Qaaf’ na ‘Dhal’ utawasikia wakisoma;
‘Iza zulzilati l ardhu’ - badala ya kusoma;
‘Idhaa zulzila’
au neno ‘Al Qalam’, wao hulitamka ‘Al Alam’
Kwa hivyo Mtume (SAW), kwa kuwaonea huruma umma wake, akamwomba Mola wake awarahisishie kwa kuwaruhusu kusoma kila kabila kwa msomo wake.
AINA YA MISOMO
Kwa mfano katika kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo;
‘Maa haadha BASHARAA – katika usomaji wa Ibni Masaood(RA), ilikuwa ikisomwa;
‘Maa haadha BASHARUN’
Katika kusoma;
‘Rabbanaa BAA- ID bayna as faarina – kwa njia ya kuomba. Wengine wakasoma;
‘Rabbanaa BA- ADA bayna as faarina - kwa njia ya kutowa habari.
Hii ni Misomo tofauti lakini bila kubadilika maana yake.
Au ‘ Yaalamun’ kusomwa ‘Taalamun’
‘WA MAA khalaqa dhakara wal untha ‘ ikasomwa;
‘WA khalaqa dhakara wal untha’
‘Jannatun TAJRIY MIN tah tiha l anhaar’ ikasomwa;
‘Jannatun TAJRIY TAH TIHA l anhaar’ bila ya neno ‘min’
‘Lahma akhiy- hi maytan FAKARIHTUMUHU’ Ibni Masaood kasoma;
‘FAKURRIHTUMUUHU’
Na maana ya mwanzo ‘huku ikikuchukiza’ na ya pili ‘ huku ukichukizwa’
Hii ni misomo mbali mbali lakini kama itakavyobadilishwa huwa haibadilishi maana ya aya.
Na Mtume(SAW) akawaambia;
‘Vyovyote mtakavyosoma ikiwa haibadiliki maana ya Rahma ikawa ghadhabu au kinyume cha hivyo basi hapana tatizo’
Mtume(SAW) aliwaruhusu kusoma hivyo kwa sababu wakati ule ilihitajika misomo ile, lakini ilipohitajika Qurani isomwe kwa msomo mmoja tu, umma wote ulikubali kufanya hivyo bila ya kukhitilafiana.
HADITHI KUHUSU ZILE ZINAZODHANIWA KUWA NI AYA YA RADHA – A (KUNYONYESHA) NA RAJM (KUPIGWA MAWE)
Pana hadithi mbili zinazowababaisha baadhi ya watu na kudhani kuwa kulikuwa na aya katika Qurani zikisomwa na baadaye zikaondolewa. Hadithi hizi zinajulikana kuwa ni za “Aya ya Radha-a na ya Rajm”.
  1. Hadithi ya Bibi Aisha iliyosimuliwa na Imam Malik isem;
    “Ilikuwa katika yyaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, ikijulikana kuharimishwa baada ya kunyonya mara kumi, ikabadilishwa kwa kunyonya mara tano na haya ndiyo yanayosomwa katika Qurani.”
    Maulamaa wanasema kuwa hadithi hii haijuzu kuifanya kama ni dalili kuwa kulikuwa na aya ya Qurani kisha ikafutwa, hasa kwa vile hadithi hii ni dhaifu kwa sababu ni katika hadithi zinazoitwa (Aahaad) yaani hadithi zilizopokelewa kwa njia ya mtu mmoja tu.
    Na Hata tukiijadili hadithi hii kwa ajili ya mjadala tu, basi natija yake itakuwa hivi;
    Hadithi inasema; ‘Ilikuwa katika yaliyoteremshwa…’ na inajulikana kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha wahyi mwengine usiokuwa Qurani kwa sababu Hadithi za Mtume(SAW) na Hadithul Qudusiy pia ni katika aliyoteremshiwa Mtume(SAW) lakini si katika Qurani.
    Mwenyezi Mungu anasema;
    "Na tumekuteremshieni mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na
    ili wapate kufikiri."
    (An - Nahli-44).
    Na Mtume(SAW) katika hadithi iliyosimuliwa na Bukhari anasema;
    “Mimi nimeteremshiwa Qurani na nyingine iliyo mfano wake pamoja nayo”.
    Na kama inavyojulikana kuwa sheria nyingi zimepokelewa kwa njia ya hadithi za Mtume(SAW).
  2. Katika hadithi nyingine yenye mfano huo ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Omar bin Khattab(RA) isemayo;
“Mwenyezi Mungu amemleta Muhammad kwa haki na akamteremshia kitabu, na katika aliyoteremshiwa ni aya ya rajm (kupiga mawe), tuliisoma na kuifahamu na tukapiga mawe, ninaogopa wakati ukipita mtu anaweza kusema;
‘Mbona hatuioni aya ya mawe katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ningekuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Omar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”
Anasema Sheikh AL Qutby Mahmoud katika kitabu chake kiitwacho ‘Mabaahith fiy Uluum l Quraan;
Sisi hatuamini kuwa Omar na Aisha(RA) wanaweza kusema maneno kama haya ingawaje hadithi hizi mbili zimo katika vitabu vya hadtihi, kwa sababu katika vitabu vya hadithi, zimo nyingi zenye udhaifu wa Isnad’
Juu ya hayo ikiwa tutaijadili hadithi hii kwa ajili ya mjadala tu , (anaendelea kusema mwanachuoni huyo) pana dalili katika kauli ya Omar(RA) kuwa hayo yaliyoteremshwa si katika Qurani na hii inatokana na pale alipoikamilisha kauli yake kwa kusema;
“Ningekuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Omar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”
Kisha hii pia ni katika hadithi za ‘Aahaad’ na siyo ‘Mutawatir’ na maana ya hadith ‘Mutawaatir’ ni Hadithi iliyosemwa na wasiopungua watu kumi katika kila tabaka la Al Ruwaat [Classes] na maana yake ni lazima wawe kumi katika tabaqa ya Masahaba na kumi katika tabaqa ya Al Tabeen na kumi katika tabaqa ya Taabea al tabeen hata ifikie daraja la kuweza kukubaliwa kuwa ni katika Qurani. Kama tutakavyoona tukiendelea na darsi hii kuwa katika ukusanyaji wa Qurani wakati wa Abubakar(RA), Zeyd(RA) akimkatalia Omar(RA) kupunguza herufi moja tu ya ‘Waaw’ katika Qurani mpaka alipoleta shahidi aliyehifadhi, bali aliyekuwa katika waandishi wa Wahyi ambaye ni Kaab(RA) na juu ya hivyo Kaab(RA), alishuhudia dhidi ya Omar(RA) na kwa ajili hiyo herufi ya ‘waaw’ ikabaki pale katika aya tatu zile.
Kwa hivyo hadithi hiyo ya Omar inayohusiana na Rajam haikuwemo katika Qurani, Kwa sababu Omar(RA) mwenyewe ametamka;
“Ningekuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Omar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”
Ikajulisha kuwa haikuwa katika Qurani.
Ama ile hadithi ya kunyonya ina mgongano mingi katika isnad yake na kwa ajili hiyo pia haiwezi kufikia daraja ya kuwa aya katika Qurani.
KUKUSANYWA KWA QURANI
Neno ‘Kukusanya’ baadhi ya wakati hutumika kwa maana ya kukusanya moyoni, kifuani au kusomwa kwa mpangilio unaotakikana, na mara nyengine linatumika kwa maana ya kuiandika.
Na kukusanywa huku kumefanyika mara tatu;
a- Wakati wa Mtume(SAW),
b- Wakati wa Abubakar(RA), na
c- Wakati wa Othman(RA).
Wakati wa Mtume(SAW), watu walikuwa wakiipenda sana Qurani na kuisoma misikitini na majumbani na walikuwa wakishindana katika kuihifadhi Qurani, hata katika baadhi ya riwaya zilizopokelewa zinasema kuwa watu walikuwa wanapo owa, mahari yao yalikuwa ni Qurani. Walikuwa wakiulizwa umehifadhi Sura fulani? Na jawabu ikiwa ‘Ndiyo’, basi huambiwa kuwa mahari yake ni kumfundisha mkewe Sura hiyo.
Na ilikuwa ni jambo la kawaida kama ilivyo sasa kuwa katika Sala, Imam anapokosea katika kusoma Qurani, hapo hapo hukosolewa na aliye nyuma yake.
Kwa hivyo wakati wa Mtume(SAW), Qurani ilikuwa ishakusanywa vifuani mwa Waislam pamoja na kuandikwa katika magamba, katika majani, makozi, mafupa n.k.
Alipokufa Mtume(SAW) watu wengi sana walikuwa washaihifadhi Qurani vifani mwao, kinyume na baadhi ya hadithi zinazosema kuwa waliohifadhi walikuwa wanne tu.
A- KUKUSANYWA KWA QURANI WAKATI WA MTUME(SAW)
Mtume(SAW) aliwachagua baadhi ya Masahaba(RA) na kuwapa kazi ya kuiandika Qurani kila anapoteremshiwa Wahyi, na Masahaba hawa(RA), walikuwa wakijulikana kuwa ni; ‘Kuttabul Wahyi’ . Na maana yake ni, ‘Waandishi wa Wahyi’.
Alikuwa mara anapoteremshiwa Wahyi na Jibril(AS), akiwaita waandishi hao na kuwaamrisha kuyaandika yale aliyofunuliwa. Bila shaka kwa vile wakati ule hakukuwa na karatasi, walikuwa wakiandika juu ya magamba, majani, mafupa nk.
Kwa hivyo Qurani iliandikwa wakati wa Mtume(SAW), na iliwekwa nyumbani kwake na ilikuwepo kwa baadhi ya Sahaba waliokuwa wakiandika Wahyi, na pia ilihifadhiwa vifuani mwa Waislam. Isipokuwa iliandikwa juu ya magamba na majani na makozi ya miti, nk. Na haikuwa imekusanywa mahala pamoja, katika kitabu kimoja kama ilivyo hivi sasa.
Mtume(SAW) alipofariki, Qurani ilikuwa ishahifadhiwa vifuani mwa Waislam na kwa mpangilio ule ule alioteremshiwa.
Imesimuliwa na Imam Ahmed bin Hanbal kuwa Othman bin Abi L Aas amesema;
“Nilikuwa nimekaa kwa Mtume(SAW), Mtume akayafumba macho yake kisha akayafumbua, kisha akasema;
“Amenijia Jibril na kuniamrisha niiweke aya hii mahala hapa katika Sura hii; (Aya yenyewe ni hii;)
‘Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na kufanya hisani na kuwapa jamaa na anakataza uchafu na uovu na dhulma. Anakunasihini ili mupate kufahamu (mfate).’
An Nahl – 90
Jibril(AS), alikuwa akimsikiliza Mtume(SAW) Qurani yote mara moja kila mwaka, na katika mwaka alofariki, Mtume(SAW) alisikilizwa na Jibril(AS) Qurani yote mara mbili. Na dalili ni hadithi iliyosimuliwa na Imam Muslim kutoka kwa Bibi Aisha(RA) aliposema;
“Tulikuwa wake za Mtume sote kwake na hakuna aliyeondoka, na Fatima(RA) akaja huku akitembea kwa mwendo wake uliokuwa kama wa babake Mtume wa Mwenyezi Mungu(SAW), na Mtume alipomwona akamkaribisha na kumwambia:
‘Karibu mwanangu’, kisha akamwambia akae kuliani au kushotoni pake, kisha akamnon’goneza, na (Fatima(RA)) (baada ya kunon’gonezwa) akalia kilio kikubwa kisha akamnon’goneza tena, na (Fatma(RA)) akacheka. Nikamwambia;
‘ Babako amekunon’goneza peke yako mbele ya wake zake wote kisha unalia?’
Na Mtume aliposimama (baada ya kujisikia vizuri kidogo) nikamuuliza (Fatima(RA));
‘Babako alikwambia nini?’
Akanijibu;
‘Siitowi siri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu’
Baada ya kufariki Mtume(SAW), (Fatima(RA) akanambia;
‘Sasa nitakwambia, ama pale aliponinong’oneza mara ya mwanzo (nikalia), alinambia kuwa; ‘Kwa kawaida Jibril hunisikiliza Qurani yote mara moja kila mwaka lakini safari hii kanisikiliza Qurani yote mara mbili, na sioni tafsiri ya kitendo hicho isipokuwa ni kuwa kifo changu kinakaribia, kwa hivyo mche Mungu na subiri kwa sababu mimi ni kizazi chema kwako kilichokutangulia’ Akasema; Ndiyo pale mliponiona nikilia, na alipoiona huzuni yangu, akaninon’goneza tena na kunambia;
‘Fatima, hutoridhika ukiwa wewe ni bibi wa wanawake wa Kiislam? Au Bibi wa wanawake wa Umma huu?’
Akasema ; Ndipo nilipocheka pale mliponiona nikicheka”.
Kutokana na dalili hii, tunatambua kuwa Qurani yote ilikuwa ishahifadhiwa tokea wakati wa Mtume(SAW), na kabla hajafariki.
Kwa hivyo Qurani ilikuwa ikifundishwa kwa mpangilio huu huu na kusomwa na kusikilizwa na Mtume(SAW), na yeye Mtume(SAW) alikuwa akisikilizwa na Jibril(AS) kila mwaka.
MASAHABA PIA WALIKUWA WAKISIKILIZWA NA MTUME(SAW) QURANI, NA AKIWATAKA WAO PIA WAMSIKILIZE
Mtume(SAW), alikuwa akisoma sura zote za Qurani kwa mpangilio huu huu katika Sala mbele ya Masahaba, na alikuwa akiwasikiliza na kuwasikilizishQurani Masahaba(RA) mbali mbali na katika nyatofauti.
Imepokelewa kuwa siku moja Mtume(SAW) alimwambia Ubay bin Kaab(RA) ;
‘Mwenyezi Mungu ameniamrisha nikusomee Qurani ‘
Ubay(RA) akauliza ;
‘Mwenyezi Mungu amenitaja kwa jina langu?’
Mtume(SAW) akamjibu;
‘Ndiyo’
Ubay(RA) akalia sana.
Mtume(SAW) alikuwa akiwasomea na kusomewa Qurani kwa ajili ya kuwafundisha Masahaba wake na kuhakikisha kuwa wameihifadhi kama inavyotakikana.
Imepokelewa pia kuwa Mtume(SAW) siku moja alimtaka Abdillahi bin Masaood(RA) amsomee Qurani, na Abdillahi(RA) akamsomea Suratul Nisaa mpaka alipofika aya ya 40 isemayo;
“Basi itakuwaje tutakapoleta shahidi katika kila uma; na tukakuleta wewe (Nabii Muhammad) uwe shahidi juu ya huu (Uma wako)?”
Alipofika hapo Mtume(SAW) akamwambia;
‘Basi, hapo hapo, inatosha’
Abillahi bin Masaood anasema;
‘Nilipomtizama nikamwona macho yake yanamlenga machozi’
Muslim.
Kwa hivyo Mtume(SAW) pia alikuwa akiwasikiliza Masahaba(RA) Qurani kwa mpangilio huu huu alofundishwa na kusikilizwa na Jibril(AS) kila mwaka.
B- KUKUSANYWA KWA QURANI WAKATI WA ABUBAKAR(RA)
Kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa Qurani iliandikwa, ilisomwa, ilikusanywa na kupangwa kama ilivyotakikana chini ya mafundisho ya Mtume(SAW), aliyekuwa akifundishwa na Jibril(AS) tokea wakati wa uhai wake.
Isipokuwa haikuwa imekusanywa katika kitabu kimoja kama ilivyo sasa, bali ilikuwa katika sehemu mbali mbali zilizokuwa zimeandikwa juu yake. Na Mtume(SAW) alizikusanya na kuzifunga au kuzishonea kwa uzi na kuziunganisha pamoja.
Katika vita vya AL Yamama vilivyotokea mwaka wa kumi na mbili baada ya Al Hijra, mwaka wa pili baada ya kufa kwa Mtume(SAW), pale Musailima l kadhaab alipojidai kuwa yeye ni mtume, waliuliwa watu waliohifadhi Qurani wapatao sabini.
Omar bin Khatab(RA) alipoona vile akamwendea Abubakar(RA) na kumshauri kuiandika na kuikusanya Qurani katika kitabu kimoja ili isije ikapotea kwa sababu ya kufa kwa walioihifadhi na pia kwa kutawanyika kwa zile sehemu zilizoandikwa ndani yake Qurani.
Na alimjulisha kuwa kitendo hicho hakitokuwa cha Uzushi (bidaa), kwa sababu Mtume(SAW) mwenyewe aliamrisha iandikwe wakati wake na pia ilikusanywa wakati wake.
Baada ya majadiliano marefu, Abubakar(RA) akaridhika na shauri la Omar(RA).
Bukhari
Anasema Zeyd bin Thabit(RA), aliyekabidhiwa jukumu hilo la kuikusanya na kuiandika akishirikiana na Masahaba wenzake waliochaguliwa kwa kazi hiyo kuwa;
“Nikaanza kukusanya kutoka katika kila sehemu iliyoandikwa na kutoka kwa watu walioihifadhi vifuani pao, mpaka nilipoipata mwisho wa Sura ya Tawba ikiwa kwa Abi Khuzayma l Ansari(RA) peke yake na hakuwa nayo mwengine isipokuwa yeye na aya yenyewe ni;
“Amekufikieni Mtume alie jinsi moja na nyinyi, yanamhuzunisha yanayokutaabisheni , anakuhangaikieni. (Na) kwa walioamini ni mpole na Mwenye huruma ….”, mpaka mwisho wa aya hiyo.”
Aya hii ilikuwa imehifadhiwa na wengi, na ilikuwemo katika ule mtungo wa maandishi aloukusanya na kuushonea Mtume(SAW), lakini haikuwa imeandikwa pengine isipokuwa kwa Sahaba huyo tu.
Baada ya kukusanywa huko, pamoja na kulinganishwa na Qurani aloikusanya Mtume(SAW) na hatimaye kuandikwa katika kitabu kimoja, msahafu huo ukawa kwa Abubakar(RA) mpaka alipofariki, kisha ukawa kwa Omar(RA), kisha ukabaki nyumba ya Hafsa bint Omar(RA).
Zeyd huyu(RA), alikuwa katika waandishi wa Wahyi na alikuwa miongoni mwa waliohifadhi Qurani, na alikuwa pia katika walioandika aya za mwisho za Qurani mbele ya Mtume(SAW).
Omar(RA) ndiye aliyetangaza akisema;
“Waandishi wa Wahyi (Kuttabul Wahyi) wote waliokuwa wakiiandika mbele ya Mtume(SAW) walete (yale waliyoandika ili tuiandike mahala pamoja)”.
Watu wakauitikia mwito huo.
Zeyd(RA), aliyepewa jukumu la kuwa kiongozi wa kuifanya kazi hiyo, hakuwa akikubali kuandika chochote isipokuwa mbele ya mashahidi wawili, (mmoja awe katika waliohifadhi na mwengine katika walioandika mbele ya Mtume(SAW)) na lazima zikubaliane kila herufi, na alikuwa kabla ya kuandika akipambanisha yale yaliyoandikwa na yale yaliyomo vifuani mwa waliohifadhi, pamoja na kuhakikisha kwa kupambanisha yaliyoandikwa hapo mwanzo na yale yaliyonukuliwa baadaye na watu wengine, yote haya ili kuhakikisha kuwa ananukuu kama inavyopaswa.
Na alikuwa hategemei hifdhi ya mtu mmoja, bali alikuwa akihakikisha kila aya kabla ya kuiandika kwa wengi miongoni mwa waliohifadhi.
Kulitokea mabishano baina ya Zeyd na Omar(RAnhum) katika herufi za ‘Waaw’ katika aya tatu zifuatazo;
Wa
Wa
Wa
Omar(RA) alikuwa akiona kwa hakukuwa na herufi ‘waaw’ na kwamba aya husomwa;
A
A
A
Lakini Zeyd(RA) hakukubali kuziandika kwa rai ya Omar, na akasema kuwa aya hizo zinasomwa kwa herufi ya ‘waaw’
Zinasomwa hivi;
Wal
Wa
Omar(RA) akasema;
‘Mwiteni Kaab’ (Huyu ni katika waandishi wa Wahyi na pia katika waliohifadhi).
Akaitwa Kaab(RA) na akashuhudia kwa kukukubaliana na Zeyd dhidi ya Omar(Ranhum), kuwa aya zote hizo husomwa na ‘waaw’.
C- KUKUSANYWA KWA QURANI WAKATI WA OTHMAN(RA)
Wakati alipotawala Othman(RA) kuwa Khalifa wa Waislam, dini ya Kiislam ilipata nguvu zaidi na Waislam waliweza kuzishinda nchi mbali mbali na kusonga mbele hadi kufikia Azarbeijan na Armenia na kuweza pia kuziteka nchi mbali mbali za Asia na za Europe.
Baadhi ya Masahaba kama vile kina Hudhaifa(RA), wakaona mambo ya kiajabu kila wakisonga mbele kuziteka nchi hizo. Katika nchi ya Syria na nchi ya Misri Waislam walikuwa wakishindana kwa kutamba, kila mmoja akisema kuwa msomo wake wa Qurani ni bora kuliko wa mwenzake na kufikia hadi kukufurishana kwa ajili hiyo.
Othman(RA) baada ya kusikia hayo, akashauriana na Masahaba wenzake na akaona kuwa ipo haja kubwa sana ya kuwaunganisha Waislam wote wawe wanaisoma Qurani kwa msomo mmoja tu na kwa kutumia herufi moja tu.
Wakakubaliana Masahaba wote(RA), kuwa wauchukue ule Msahafu uliokusanywa na Abubakar(RA), na kuunukuu kwa kuuandika tena katika misahafu mingine mingi, na wakakubaliana kuwa itumike lugha ile ile ya ki Qureshi ambayo ndiyo iliyoteremshiwa Qurani, kisha waisambaze misahafu hiyo kila pahali katika nchi za Kiislam na kuichoma moto yote iliyobaki iliyoandikwa kwa misomo tofauti, ili kuikata mizizi ya fitna kuanzia chanzo chake, mizizi ambayo inge endelea, Mwenyezi Mungu tu ndiye ajuaye mwisho wake.
Ikachaguliwe tume ya waliohifadhi Qurani pamoja na wajuzi wa lugha na Othman(RA) aliwaambia;
‘Iwapo itatokea khitilafu yoyote juu ya neno lolote basi liandikeni kwa lugha ya ki Qureshi’
Baada ya kukamilika kazi hiyo, akaurudisha ule wa Abubakar(RA) nyumbani kwa Hafsa(RA).
Haya yalifanywa baada ya kupatikana makubaliano baina ya Umma wote kuwa ipo haja kubwa ya kufanya hivyo.
Sayiduna Ali(RA) alipowasikia baadhi ya watu wakimlaumu Othman(RA) kuwa amechoma moto Qurani, aliwaambia;
“Mcheni Mola wenu enyi watu, msipindukie mipaka katika kumlaumu Othman na kusema kuwa eti yeye ni mchomaji wa misahafu, kwani Wallahi misahafu imechomwa mbele ya Masahaba wote na baada ya kukubaliana sote. Na mimi ningelikuwa Amiri, basi ningefanya kama alivyofanya”.
Kwa hivyo Abubakar(RA) aliikusanya na kuiandika Qurani kwa kuogopa isipotee kwa sababu ya kufa kwa waliohifadhi, ama Othman(RA), aliiandika na kuichoma iliyobaki kwa kuogopa mfarakano.
Lakini Qurani aloiandika Othman(RA), ni ile ile aloiandika Abubakar(RA), aliyoinukuu kutoka katika ile iliyoandikwa mbele ya Mtume(SAW) na kuhifadhiwa kwake(SAW).
Mtu anaweza kuuliza;
‘Kwa nini Othman ameacha kukiendeleza kitendo alichofanya Mtume(SAW) cha kuisoma Qurani kwa misomo mingi?
Jibu;
Kwa sababu Mtume(SAW), hakuamrisha hivyo, bali alipendekeza tu, kwa sababu wakati ule ilikuwepo haja ya kuwafundisha watu kusoma Qurani kwa misomo yao mbali mbali, lakini wakati wa Othman(RA) ilikuwepo haja ya kuwaunganisha Waislam kwa msomo mmoja tu na katika msahafu mmoja.
Na kama inavyojulikana kuwa katika hadithi iliyosimuliwa na Imam Ahmed , Ibni Majah, Attirmidhy na kwa njia nyingi kuwa Mtume(SAW) ametuamrisha kuwa tutakapoona khitilafu nyingi, basi tufuate mafundisho yake na mafundisho ya Makhulafaa al Raashidiyn watakaokuja baada yak.
Na Othman(RA) ni katika hao Makhulafaa Al Rashidiyn.
aakhariyna
ladhyna
lladhiyna jaauw min ba-adihim
akhariyna minhum lamma yal haku bihim – na
lladhiyna ttabauuhum bi ihsanin – na
lladhiyna jaauw min baadihim
aakhariyna minhum lamma yal haku bihim – na
llahdhiyna tabauuhum bi ihsanin – na