بسم الله الرحمن الرحيم


بسم الله الرحمن الرحيم

UDOMSA.

Wednesday, 15 September 2010

ELIMU YA KURAN-ULUMU L QUR – AN


ULUMU L QUR – AN
Ulumul Qur – an, maana yake ni ‘Elimu inayohusiana na Qurani’, na elimu yenyewe sio ya tafsiri ya Qurani, bali ni elimu inayohusiana na kuijuwa Qurani, maana yake, vipi imeshuka, aya gani zilizotangulia na zipi zilizoteremshwa baadaye, sura ipi Iliyoteremshwa Makka na ipi ya Madina, aya ipi iliyofutwa na ipi iliyofuta, vipi imekusanywa na kuandikwa na mambo mengi mengine.
Imam Shafi (Rahimahu llah) alipoletwa mbele ya Khalifa wa Waislam Harun Al Rashid baada ya kusingiziwa uongo na Amiri aliyekuwa akitawala wakati huo huko Yemen, aliletwa akiwa amefungwa minyororo hadi shingoni pake.
Baada ya kuulizwa masuali mengi na Khalifa huyo akamtaka aelezee nini anachojuwa kuhusu Elimu ya Qurani.
Imam Shafi akajibu;
“Hakika Elimu za Qurani ni nyingi, je! Unaniuliza juu ya aya zisizobeba isipokuwa maana moja tu (Muhkam) au zinazobeba maana zaidi ya moja (Mutashabih) au ipi iliyotangulia na ipi iliyokuja baada yake (Taqdiym na Taakhiyr) au unataka kujuwa ipi iliyofutwa na ipi iliyofuta (Nasikh na Mansukh) au juu ya ………?”
Akaendelea hivyo huku akijibu kila suala analoulizwa na Harun AL Rashiyd mpaka Khalifa huyo akahakikisha kuwa huyu ni Alim wa kweli, akaamua afunguliwe na kupewa heshima zote wanazopewa Maulamaa.
MFANO WA AYA ZILIZOFUTA NA ZILIZOFUTWA (NASIKH NA MANSUKH)
Mwenyezi Mungu anasema;
“Aya yo yote tunayoifuta au kuisahahuliza tunaleta iliyo bora kuliko hiyo au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu?”.
Al Baqarah- 106
Imam AL Shafi-i (Rahimahullah) anasema;
“Mwenyezi Mungu hafuti hukmu isipokuwa ataleta badala yake hukmu nyingine. Mfano pale alipoifuta hukmu ya kuelekea Baytul Maqdis katika Sala na akaileta badala yake hukmu ya kuelekea Al Kaaba”.
Imam Shafi akiendelea kutoa mifano alisema;
“Mwenyezi Mungu anasema;
“Ewe Mtume (wa Mwenyezi Mungu)! Wahimize walioamini wende vitani. Wakipatikana kwenu watu ishirini wanaousubiri watashinda mia mbili (katika hao makafiri. Basi nyinyi mkiwa ishirini lazima msimame mupigane na watu miteni).
Na kama wakiwa watu mia moja kwenu watashinda elfu moja ya wale waliokufuru, maana hao ni watu wasofahamu. (Basi watu mia katika nyinyi wasiwakimbie watu elfu katika wao)”
AL Anfal – 65
Katika aya hii Mwenyezi Mungu anatujulisha kuwa Waisalm wanazo nguvu za Imani kiasi ambapo Waislam ishirini wanaweza kupigana na makafiri mia mbili na kwamba Mwislam mmoja anatakiwa asikimbie akipambana na makafiri kumi.
Lakini baada ya Mwenyezi Mungu kuona kuwa upo udhaifu, na hii inatokana na vita kuendelea mda mrefu, Mwenyezi Mungu akapunguza pia idadi, kwa kutujulisha kuwa sasa Waislam mia moja wanaweza kuwashinda makafiri mia mbili. Muislam mmoja anatakiwa asikimbie akipigana na makafiri wawili.
Mwenyezi Mungu anasema;
“Sasa Mwenyezi Mungu amekukhafifishieni maana anajua ya kwamba kuna udhaifu (sasa) kwenu (kwa kuwa vita vimeendelea kwa mda mrefu). Kwa hivyo wakiwa watu mia moja kwenu wenye subira na wawashinde watu mia mbili kwao; na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu nawawashinde elfu mbili; kwa amri yaMwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri (yaani sasa wanaambiwa kila Muislam mmoja akabiliane na makafiri wawili)”.
AL Anfal – 66
Hii ni mifano miwili katika kuisherehesha maana ya kufutwa aya na kuletwa nyingine badala yake, na tumeona kuwa; Aya yoyote inapofutwa haina maana kuwa haisomwi tena, bali inasomwa kama Aya nyingine isipokuwa hukmu yake hubadilishwa kwa hukmu nyingine.
Ingawaje Elimu za Qurani ni nyingi na zina mpangilio wake maalum wa kuandikwa, lakini leo sitoanza kwa mpangilio huo na badala yake nitazungumza moja kwa moja juu ya jambo linalotohusu zaidi kwa wakati huu, nalo ni;
Kuteremshwa Qurani kwa herufi saba na jinsi ilivyoandikwa na kukusanywa wakati wa Mtume(SAW) na jinsi ilivyokusanywa wakati wa Abubakar(RA) na hatimaye wakati wa Othman(RA)”.
Kabla ya yote ningependa tutambue kuwa Itikadi yetu ni kuwa; Hatuamini kuwa kulikuwa na aya yoyote au hata herufi moja iliyoondolewa kutoka katika Qurani, bali tunaamini kuwa msahafu huu tunaousoma sasa na yale yaliyomo ndani yake ni yale yale yaliyokuwemo tokea wakati wa Mtume(SAW) alipokuwa akiishi na akiteremshiwa Wahyi.
Isipokuwa pana tofauti ya misomo (Qira aat) na pia pana hadithi mbili zinazowababaisha baadhi ya watu na kufikiria kuwa kulikuwa na Aya mbili ndani ya Qurani na kwamba sasa hazipo tena. Aya hizi zinajulikana kama ifuatavyo;
a- Ayatul Rajm
b- Ayatul Ridha a.
Baadhi ya watu walidhania kuwa hizi ni Aya na kwamba zilikuwemo ndani ya Qurani, na Inshaallah kila tunapoendelea mbele na darsi hii tutatambua ukweli kuwa hizo si Aya na wala hazikuwemo ndani ya Qurani.
KUTEREMSHWA QURANI KWA MISOMO SABA
Mtume(SAW) aliteremshiwa Qurani kwa misomo saba. Hadithi nyingi zilizo sahihi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume(SAW), zinasema kuwa Jibril(AS) alimsomesha Mtume(SAW) Qurani kwa msomo wa aina moja, kwa lugha ya ki Qureshi, lakini Mtume(SAW) alimtaka Jibril(AS) amuombe Mwenyezi Mungu iongezwe misomo mingi zaidi kwa sababu wakati ule Waislam wepya walikuwa wengi na wangepata taabu sana kuifaham Qurani kwa msomo wa lugha moja ya ki Qureshi peke yake, hasa kwa vile walikuwa wapo watu wa tabaka mbali mbali, makabila mbali mbali na kutoka mataifa mbali mbali.
Mtume(SAW) anasema;
“Jibril alinisomea Qurani kwa herufi (msomo wa aina) moja, nikamwambia aniongezee mpaka ikafikia misomo saba”
Bukhari na Muslim
Waarabu katika lugha yao wana misemo mbali mbali, isipokuwa lugha ya ki Qureshi ndiyo iliyokuwa ikitumika zaidi, na ndiyo iliyoandikiwa Qurani, na hii inatokana na kuwa wao ndio walinzi wa Nyumba kongwe (Al Kaaba), na wao ndio waliokuwa wakiwahudumia Mahujaji hata kabla ya kuja Uisalmu.
Katika lugha ya Kiswahili kwa mfano, utakuta misemo ya aina mbali mbali, ikibeba maana moja.
Tanzania bara utakuta herufi R inatamkwa L na herufi L inatamkwa R. ‘Nyanya’ inaitwa ‘tungule’ na tungule inaitwa ‘nyanya’.
Ama Kenya, neno ‘njoo’ wanasema ‘ndoo’ na katika kiswahili cha Tanzania neno ‘ndoo’ ni ile inayotekewa maji. Bali wakati mwingine utakuta neno kamili hubadilika kwa mfano neno ‘kuhama’ kule Kenya wanaita ‘kugura’.
Na hivi ndivyo ilivyo katika lugha ya kiarabu, kwa mfano neno mpira huitwa ‘Kurra’ lakini ukenda Yemen katika mji wa Aden, mpira unaitwa ‘kubba’ na sio ‘kurra’, na ukiondoka hapo Aden na kuelekea Hadhramout utaona kuwa neno ‘kubba’ maana yake ‘kaburi’.
Na Masri pia kuna matatizo yake, hasa katika kuitamka herufi ‘Qaaf’ na ‘Dhal’ utawasikia wakisoma;
‘Iza zulzilati l ardhu’ - badala ya kusoma;
‘Idhaa zulzila’
au neno ‘Al Qalam’, wao hulitamka ‘Al Alam’
Kwa hivyo Mtume (SAW), kwa kuwaonea huruma umma wake, akamwomba Mola wake awarahisishie kwa kuwaruhusu kusoma kila kabila kwa msomo wake.
AINA YA MISOMO
Kwa mfano katika kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo;
‘Maa haadha BASHARAA – katika usomaji wa Ibni Masaood(RA), ilikuwa ikisomwa;
‘Maa haadha BASHARUN’
Katika kusoma;
‘Rabbanaa BAA- ID bayna as faarina – kwa njia ya kuomba. Wengine wakasoma;
‘Rabbanaa BA- ADA bayna as faarina - kwa njia ya kutowa habari.
Hii ni Misomo tofauti lakini bila kubadilika maana yake.
Au ‘ Yaalamun’ kusomwa ‘Taalamun’
‘WA MAA khalaqa dhakara wal untha ‘ ikasomwa;
‘WA khalaqa dhakara wal untha’
‘Jannatun TAJRIY MIN tah tiha l anhaar’ ikasomwa;
‘Jannatun TAJRIY TAH TIHA l anhaar’ bila ya neno ‘min’
‘Lahma akhiy- hi maytan FAKARIHTUMUHU’ Ibni Masaood kasoma;
‘FAKURRIHTUMUUHU’
Na maana ya mwanzo ‘huku ikikuchukiza’ na ya pili ‘ huku ukichukizwa’
Hii ni misomo mbali mbali lakini kama itakavyobadilishwa huwa haibadilishi maana ya aya.
Na Mtume(SAW) akawaambia;
‘Vyovyote mtakavyosoma ikiwa haibadiliki maana ya Rahma ikawa ghadhabu au kinyume cha hivyo basi hapana tatizo’
Mtume(SAW) aliwaruhusu kusoma hivyo kwa sababu wakati ule ilihitajika misomo ile, lakini ilipohitajika Qurani isomwe kwa msomo mmoja tu, umma wote ulikubali kufanya hivyo bila ya kukhitilafiana.
HADITHI KUHUSU ZILE ZINAZODHANIWA KUWA NI AYA YA RADHA – A (KUNYONYESHA) NA RAJM (KUPIGWA MAWE)
Pana hadithi mbili zinazowababaisha baadhi ya watu na kudhani kuwa kulikuwa na aya katika Qurani zikisomwa na baadaye zikaondolewa. Hadithi hizi zinajulikana kuwa ni za “Aya ya Radha-a na ya Rajm”.
  1. Hadithi ya Bibi Aisha iliyosimuliwa na Imam Malik isem;
    “Ilikuwa katika yyaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, ikijulikana kuharimishwa baada ya kunyonya mara kumi, ikabadilishwa kwa kunyonya mara tano na haya ndiyo yanayosomwa katika Qurani.”
    Maulamaa wanasema kuwa hadithi hii haijuzu kuifanya kama ni dalili kuwa kulikuwa na aya ya Qurani kisha ikafutwa, hasa kwa vile hadithi hii ni dhaifu kwa sababu ni katika hadithi zinazoitwa (Aahaad) yaani hadithi zilizopokelewa kwa njia ya mtu mmoja tu.
    Na Hata tukiijadili hadithi hii kwa ajili ya mjadala tu, basi natija yake itakuwa hivi;
    Hadithi inasema; ‘Ilikuwa katika yaliyoteremshwa…’ na inajulikana kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha wahyi mwengine usiokuwa Qurani kwa sababu Hadithi za Mtume(SAW) na Hadithul Qudusiy pia ni katika aliyoteremshiwa Mtume(SAW) lakini si katika Qurani.
    Mwenyezi Mungu anasema;
    "Na tumekuteremshieni mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na
    ili wapate kufikiri."
    (An - Nahli-44).
    Na Mtume(SAW) katika hadithi iliyosimuliwa na Bukhari anasema;
    “Mimi nimeteremshiwa Qurani na nyingine iliyo mfano wake pamoja nayo”.
    Na kama inavyojulikana kuwa sheria nyingi zimepokelewa kwa njia ya hadithi za Mtume(SAW).
  2. Katika hadithi nyingine yenye mfano huo ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Omar bin Khattab(RA) isemayo;
“Mwenyezi Mungu amemleta Muhammad kwa haki na akamteremshia kitabu, na katika aliyoteremshiwa ni aya ya rajm (kupiga mawe), tuliisoma na kuifahamu na tukapiga mawe, ninaogopa wakati ukipita mtu anaweza kusema;
‘Mbona hatuioni aya ya mawe katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ningekuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Omar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”
Anasema Sheikh AL Qutby Mahmoud katika kitabu chake kiitwacho ‘Mabaahith fiy Uluum l Quraan;
Sisi hatuamini kuwa Omar na Aisha(RA) wanaweza kusema maneno kama haya ingawaje hadithi hizi mbili zimo katika vitabu vya hadtihi, kwa sababu katika vitabu vya hadithi, zimo nyingi zenye udhaifu wa Isnad’
Juu ya hayo ikiwa tutaijadili hadithi hii kwa ajili ya mjadala tu , (anaendelea kusema mwanachuoni huyo) pana dalili katika kauli ya Omar(RA) kuwa hayo yaliyoteremshwa si katika Qurani na hii inatokana na pale alipoikamilisha kauli yake kwa kusema;
“Ningekuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Omar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”
Kisha hii pia ni katika hadithi za ‘Aahaad’ na siyo ‘Mutawatir’ na maana ya hadith ‘Mutawaatir’ ni Hadithi iliyosemwa na wasiopungua watu kumi katika kila tabaka la Al Ruwaat [Classes] na maana yake ni lazima wawe kumi katika tabaqa ya Masahaba na kumi katika tabaqa ya Al Tabeen na kumi katika tabaqa ya Taabea al tabeen hata ifikie daraja la kuweza kukubaliwa kuwa ni katika Qurani. Kama tutakavyoona tukiendelea na darsi hii kuwa katika ukusanyaji wa Qurani wakati wa Abubakar(RA), Zeyd(RA) akimkatalia Omar(RA) kupunguza herufi moja tu ya ‘Waaw’ katika Qurani mpaka alipoleta shahidi aliyehifadhi, bali aliyekuwa katika waandishi wa Wahyi ambaye ni Kaab(RA) na juu ya hivyo Kaab(RA), alishuhudia dhidi ya Omar(RA) na kwa ajili hiyo herufi ya ‘waaw’ ikabaki pale katika aya tatu zile.
Kwa hivyo hadithi hiyo ya Omar inayohusiana na Rajam haikuwemo katika Qurani, Kwa sababu Omar(RA) mwenyewe ametamka;
“Ningekuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Omar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”
Ikajulisha kuwa haikuwa katika Qurani.
Ama ile hadithi ya kunyonya ina mgongano mingi katika isnad yake na kwa ajili hiyo pia haiwezi kufikia daraja ya kuwa aya katika Qurani.
KUKUSANYWA KWA QURANI
Neno ‘Kukusanya’ baadhi ya wakati hutumika kwa maana ya kukusanya moyoni, kifuani au kusomwa kwa mpangilio unaotakikana, na mara nyengine linatumika kwa maana ya kuiandika.
Na kukusanywa huku kumefanyika mara tatu;
a- Wakati wa Mtume(SAW),
b- Wakati wa Abubakar(RA), na
c- Wakati wa Othman(RA).
Wakati wa Mtume(SAW), watu walikuwa wakiipenda sana Qurani na kuisoma misikitini na majumbani na walikuwa wakishindana katika kuihifadhi Qurani, hata katika baadhi ya riwaya zilizopokelewa zinasema kuwa watu walikuwa wanapo owa, mahari yao yalikuwa ni Qurani. Walikuwa wakiulizwa umehifadhi Sura fulani? Na jawabu ikiwa ‘Ndiyo’, basi huambiwa kuwa mahari yake ni kumfundisha mkewe Sura hiyo.
Na ilikuwa ni jambo la kawaida kama ilivyo sasa kuwa katika Sala, Imam anapokosea katika kusoma Qurani, hapo hapo hukosolewa na aliye nyuma yake.
Kwa hivyo wakati wa Mtume(SAW), Qurani ilikuwa ishakusanywa vifuani mwa Waislam pamoja na kuandikwa katika magamba, katika majani, makozi, mafupa n.k.
Alipokufa Mtume(SAW) watu wengi sana walikuwa washaihifadhi Qurani vifani mwao, kinyume na baadhi ya hadithi zinazosema kuwa waliohifadhi walikuwa wanne tu.
A- KUKUSANYWA KWA QURANI WAKATI WA MTUME(SAW)
Mtume(SAW) aliwachagua baadhi ya Masahaba(RA) na kuwapa kazi ya kuiandika Qurani kila anapoteremshiwa Wahyi, na Masahaba hawa(RA), walikuwa wakijulikana kuwa ni; ‘Kuttabul Wahyi’ . Na maana yake ni, ‘Waandishi wa Wahyi’.
Alikuwa mara anapoteremshiwa Wahyi na Jibril(AS), akiwaita waandishi hao na kuwaamrisha kuyaandika yale aliyofunuliwa. Bila shaka kwa vile wakati ule hakukuwa na karatasi, walikuwa wakiandika juu ya magamba, majani, mafupa nk.
Kwa hivyo Qurani iliandikwa wakati wa Mtume(SAW), na iliwekwa nyumbani kwake na ilikuwepo kwa baadhi ya Sahaba waliokuwa wakiandika Wahyi, na pia ilihifadhiwa vifuani mwa Waislam. Isipokuwa iliandikwa juu ya magamba na majani na makozi ya miti, nk. Na haikuwa imekusanywa mahala pamoja, katika kitabu kimoja kama ilivyo hivi sasa.
Mtume(SAW) alipofariki, Qurani ilikuwa ishahifadhiwa vifuani mwa Waislam na kwa mpangilio ule ule alioteremshiwa.
Imesimuliwa na Imam Ahmed bin Hanbal kuwa Othman bin Abi L Aas amesema;
“Nilikuwa nimekaa kwa Mtume(SAW), Mtume akayafumba macho yake kisha akayafumbua, kisha akasema;
“Amenijia Jibril na kuniamrisha niiweke aya hii mahala hapa katika Sura hii; (Aya yenyewe ni hii;)
‘Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na kufanya hisani na kuwapa jamaa na anakataza uchafu na uovu na dhulma. Anakunasihini ili mupate kufahamu (mfate).’
An Nahl – 90
Jibril(AS), alikuwa akimsikiliza Mtume(SAW) Qurani yote mara moja kila mwaka, na katika mwaka alofariki, Mtume(SAW) alisikilizwa na Jibril(AS) Qurani yote mara mbili. Na dalili ni hadithi iliyosimuliwa na Imam Muslim kutoka kwa Bibi Aisha(RA) aliposema;
“Tulikuwa wake za Mtume sote kwake na hakuna aliyeondoka, na Fatima(RA) akaja huku akitembea kwa mwendo wake uliokuwa kama wa babake Mtume wa Mwenyezi Mungu(SAW), na Mtume alipomwona akamkaribisha na kumwambia:
‘Karibu mwanangu’, kisha akamwambia akae kuliani au kushotoni pake, kisha akamnon’goneza, na (Fatima(RA)) (baada ya kunon’gonezwa) akalia kilio kikubwa kisha akamnon’goneza tena, na (Fatma(RA)) akacheka. Nikamwambia;
‘ Babako amekunon’goneza peke yako mbele ya wake zake wote kisha unalia?’
Na Mtume aliposimama (baada ya kujisikia vizuri kidogo) nikamuuliza (Fatima(RA));
‘Babako alikwambia nini?’
Akanijibu;
‘Siitowi siri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu’
Baada ya kufariki Mtume(SAW), (Fatima(RA) akanambia;
‘Sasa nitakwambia, ama pale aliponinong’oneza mara ya mwanzo (nikalia), alinambia kuwa; ‘Kwa kawaida Jibril hunisikiliza Qurani yote mara moja kila mwaka lakini safari hii kanisikiliza Qurani yote mara mbili, na sioni tafsiri ya kitendo hicho isipokuwa ni kuwa kifo changu kinakaribia, kwa hivyo mche Mungu na subiri kwa sababu mimi ni kizazi chema kwako kilichokutangulia’ Akasema; Ndiyo pale mliponiona nikilia, na alipoiona huzuni yangu, akaninon’goneza tena na kunambia;
‘Fatima, hutoridhika ukiwa wewe ni bibi wa wanawake wa Kiislam? Au Bibi wa wanawake wa Umma huu?’
Akasema ; Ndipo nilipocheka pale mliponiona nikicheka”.
Kutokana na dalili hii, tunatambua kuwa Qurani yote ilikuwa ishahifadhiwa tokea wakati wa Mtume(SAW), na kabla hajafariki.
Kwa hivyo Qurani ilikuwa ikifundishwa kwa mpangilio huu huu na kusomwa na kusikilizwa na Mtume(SAW), na yeye Mtume(SAW) alikuwa akisikilizwa na Jibril(AS) kila mwaka.
MASAHABA PIA WALIKUWA WAKISIKILIZWA NA MTUME(SAW) QURANI, NA AKIWATAKA WAO PIA WAMSIKILIZE
Mtume(SAW), alikuwa akisoma sura zote za Qurani kwa mpangilio huu huu katika Sala mbele ya Masahaba, na alikuwa akiwasikiliza na kuwasikilizishQurani Masahaba(RA) mbali mbali na katika nyatofauti.
Imepokelewa kuwa siku moja Mtume(SAW) alimwambia Ubay bin Kaab(RA) ;
‘Mwenyezi Mungu ameniamrisha nikusomee Qurani ‘
Ubay(RA) akauliza ;
‘Mwenyezi Mungu amenitaja kwa jina langu?’
Mtume(SAW) akamjibu;
‘Ndiyo’
Ubay(RA) akalia sana.
Mtume(SAW) alikuwa akiwasomea na kusomewa Qurani kwa ajili ya kuwafundisha Masahaba wake na kuhakikisha kuwa wameihifadhi kama inavyotakikana.
Imepokelewa pia kuwa Mtume(SAW) siku moja alimtaka Abdillahi bin Masaood(RA) amsomee Qurani, na Abdillahi(RA) akamsomea Suratul Nisaa mpaka alipofika aya ya 40 isemayo;
“Basi itakuwaje tutakapoleta shahidi katika kila uma; na tukakuleta wewe (Nabii Muhammad) uwe shahidi juu ya huu (Uma wako)?”
Alipofika hapo Mtume(SAW) akamwambia;
‘Basi, hapo hapo, inatosha’
Abillahi bin Masaood anasema;
‘Nilipomtizama nikamwona macho yake yanamlenga machozi’
Muslim.
Kwa hivyo Mtume(SAW) pia alikuwa akiwasikiliza Masahaba(RA) Qurani kwa mpangilio huu huu alofundishwa na kusikilizwa na Jibril(AS) kila mwaka.
B- KUKUSANYWA KWA QURANI WAKATI WA ABUBAKAR(RA)
Kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa Qurani iliandikwa, ilisomwa, ilikusanywa na kupangwa kama ilivyotakikana chini ya mafundisho ya Mtume(SAW), aliyekuwa akifundishwa na Jibril(AS) tokea wakati wa uhai wake.
Isipokuwa haikuwa imekusanywa katika kitabu kimoja kama ilivyo sasa, bali ilikuwa katika sehemu mbali mbali zilizokuwa zimeandikwa juu yake. Na Mtume(SAW) alizikusanya na kuzifunga au kuzishonea kwa uzi na kuziunganisha pamoja.
Katika vita vya AL Yamama vilivyotokea mwaka wa kumi na mbili baada ya Al Hijra, mwaka wa pili baada ya kufa kwa Mtume(SAW), pale Musailima l kadhaab alipojidai kuwa yeye ni mtume, waliuliwa watu waliohifadhi Qurani wapatao sabini.
Omar bin Khatab(RA) alipoona vile akamwendea Abubakar(RA) na kumshauri kuiandika na kuikusanya Qurani katika kitabu kimoja ili isije ikapotea kwa sababu ya kufa kwa walioihifadhi na pia kwa kutawanyika kwa zile sehemu zilizoandikwa ndani yake Qurani.
Na alimjulisha kuwa kitendo hicho hakitokuwa cha Uzushi (bidaa), kwa sababu Mtume(SAW) mwenyewe aliamrisha iandikwe wakati wake na pia ilikusanywa wakati wake.
Baada ya majadiliano marefu, Abubakar(RA) akaridhika na shauri la Omar(RA).
Bukhari
Anasema Zeyd bin Thabit(RA), aliyekabidhiwa jukumu hilo la kuikusanya na kuiandika akishirikiana na Masahaba wenzake waliochaguliwa kwa kazi hiyo kuwa;
“Nikaanza kukusanya kutoka katika kila sehemu iliyoandikwa na kutoka kwa watu walioihifadhi vifuani pao, mpaka nilipoipata mwisho wa Sura ya Tawba ikiwa kwa Abi Khuzayma l Ansari(RA) peke yake na hakuwa nayo mwengine isipokuwa yeye na aya yenyewe ni;
“Amekufikieni Mtume alie jinsi moja na nyinyi, yanamhuzunisha yanayokutaabisheni , anakuhangaikieni. (Na) kwa walioamini ni mpole na Mwenye huruma ….”, mpaka mwisho wa aya hiyo.”
Aya hii ilikuwa imehifadhiwa na wengi, na ilikuwemo katika ule mtungo wa maandishi aloukusanya na kuushonea Mtume(SAW), lakini haikuwa imeandikwa pengine isipokuwa kwa Sahaba huyo tu.
Baada ya kukusanywa huko, pamoja na kulinganishwa na Qurani aloikusanya Mtume(SAW) na hatimaye kuandikwa katika kitabu kimoja, msahafu huo ukawa kwa Abubakar(RA) mpaka alipofariki, kisha ukawa kwa Omar(RA), kisha ukabaki nyumba ya Hafsa bint Omar(RA).
Zeyd huyu(RA), alikuwa katika waandishi wa Wahyi na alikuwa miongoni mwa waliohifadhi Qurani, na alikuwa pia katika walioandika aya za mwisho za Qurani mbele ya Mtume(SAW).
Omar(RA) ndiye aliyetangaza akisema;
“Waandishi wa Wahyi (Kuttabul Wahyi) wote waliokuwa wakiiandika mbele ya Mtume(SAW) walete (yale waliyoandika ili tuiandike mahala pamoja)”.
Watu wakauitikia mwito huo.
Zeyd(RA), aliyepewa jukumu la kuwa kiongozi wa kuifanya kazi hiyo, hakuwa akikubali kuandika chochote isipokuwa mbele ya mashahidi wawili, (mmoja awe katika waliohifadhi na mwengine katika walioandika mbele ya Mtume(SAW)) na lazima zikubaliane kila herufi, na alikuwa kabla ya kuandika akipambanisha yale yaliyoandikwa na yale yaliyomo vifuani mwa waliohifadhi, pamoja na kuhakikisha kwa kupambanisha yaliyoandikwa hapo mwanzo na yale yaliyonukuliwa baadaye na watu wengine, yote haya ili kuhakikisha kuwa ananukuu kama inavyopaswa.
Na alikuwa hategemei hifdhi ya mtu mmoja, bali alikuwa akihakikisha kila aya kabla ya kuiandika kwa wengi miongoni mwa waliohifadhi.
Kulitokea mabishano baina ya Zeyd na Omar(RAnhum) katika herufi za ‘Waaw’ katika aya tatu zifuatazo;
Wa
Wa
Wa
Omar(RA) alikuwa akiona kwa hakukuwa na herufi ‘waaw’ na kwamba aya husomwa;
A
A
A
Lakini Zeyd(RA) hakukubali kuziandika kwa rai ya Omar, na akasema kuwa aya hizo zinasomwa kwa herufi ya ‘waaw’
Zinasomwa hivi;
Wal
Wa
Omar(RA) akasema;
‘Mwiteni Kaab’ (Huyu ni katika waandishi wa Wahyi na pia katika waliohifadhi).
Akaitwa Kaab(RA) na akashuhudia kwa kukukubaliana na Zeyd dhidi ya Omar(Ranhum), kuwa aya zote hizo husomwa na ‘waaw’.
C- KUKUSANYWA KWA QURANI WAKATI WA OTHMAN(RA)
Wakati alipotawala Othman(RA) kuwa Khalifa wa Waislam, dini ya Kiislam ilipata nguvu zaidi na Waislam waliweza kuzishinda nchi mbali mbali na kusonga mbele hadi kufikia Azarbeijan na Armenia na kuweza pia kuziteka nchi mbali mbali za Asia na za Europe.
Baadhi ya Masahaba kama vile kina Hudhaifa(RA), wakaona mambo ya kiajabu kila wakisonga mbele kuziteka nchi hizo. Katika nchi ya Syria na nchi ya Misri Waislam walikuwa wakishindana kwa kutamba, kila mmoja akisema kuwa msomo wake wa Qurani ni bora kuliko wa mwenzake na kufikia hadi kukufurishana kwa ajili hiyo.
Othman(RA) baada ya kusikia hayo, akashauriana na Masahaba wenzake na akaona kuwa ipo haja kubwa sana ya kuwaunganisha Waislam wote wawe wanaisoma Qurani kwa msomo mmoja tu na kwa kutumia herufi moja tu.
Wakakubaliana Masahaba wote(RA), kuwa wauchukue ule Msahafu uliokusanywa na Abubakar(RA), na kuunukuu kwa kuuandika tena katika misahafu mingine mingi, na wakakubaliana kuwa itumike lugha ile ile ya ki Qureshi ambayo ndiyo iliyoteremshiwa Qurani, kisha waisambaze misahafu hiyo kila pahali katika nchi za Kiislam na kuichoma moto yote iliyobaki iliyoandikwa kwa misomo tofauti, ili kuikata mizizi ya fitna kuanzia chanzo chake, mizizi ambayo inge endelea, Mwenyezi Mungu tu ndiye ajuaye mwisho wake.
Ikachaguliwe tume ya waliohifadhi Qurani pamoja na wajuzi wa lugha na Othman(RA) aliwaambia;
‘Iwapo itatokea khitilafu yoyote juu ya neno lolote basi liandikeni kwa lugha ya ki Qureshi’
Baada ya kukamilika kazi hiyo, akaurudisha ule wa Abubakar(RA) nyumbani kwa Hafsa(RA).
Haya yalifanywa baada ya kupatikana makubaliano baina ya Umma wote kuwa ipo haja kubwa ya kufanya hivyo.
Sayiduna Ali(RA) alipowasikia baadhi ya watu wakimlaumu Othman(RA) kuwa amechoma moto Qurani, aliwaambia;
“Mcheni Mola wenu enyi watu, msipindukie mipaka katika kumlaumu Othman na kusema kuwa eti yeye ni mchomaji wa misahafu, kwani Wallahi misahafu imechomwa mbele ya Masahaba wote na baada ya kukubaliana sote. Na mimi ningelikuwa Amiri, basi ningefanya kama alivyofanya”.
Kwa hivyo Abubakar(RA) aliikusanya na kuiandika Qurani kwa kuogopa isipotee kwa sababu ya kufa kwa waliohifadhi, ama Othman(RA), aliiandika na kuichoma iliyobaki kwa kuogopa mfarakano.
Lakini Qurani aloiandika Othman(RA), ni ile ile aloiandika Abubakar(RA), aliyoinukuu kutoka katika ile iliyoandikwa mbele ya Mtume(SAW) na kuhifadhiwa kwake(SAW).
Mtu anaweza kuuliza;
‘Kwa nini Othman ameacha kukiendeleza kitendo alichofanya Mtume(SAW) cha kuisoma Qurani kwa misomo mingi?
Jibu;
Kwa sababu Mtume(SAW), hakuamrisha hivyo, bali alipendekeza tu, kwa sababu wakati ule ilikuwepo haja ya kuwafundisha watu kusoma Qurani kwa misomo yao mbali mbali, lakini wakati wa Othman(RA) ilikuwepo haja ya kuwaunganisha Waislam kwa msomo mmoja tu na katika msahafu mmoja.
Na kama inavyojulikana kuwa katika hadithi iliyosimuliwa na Imam Ahmed , Ibni Majah, Attirmidhy na kwa njia nyingi kuwa Mtume(SAW) ametuamrisha kuwa tutakapoona khitilafu nyingi, basi tufuate mafundisho yake na mafundisho ya Makhulafaa al Raashidiyn watakaokuja baada yak.
Na Othman(RA) ni katika hao Makhulafaa Al Rashidiyn.
aakhariyna
ladhyna
lladhiyna jaauw min ba-adihim
akhariyna minhum lamma yal haku bihim – na
lladhiyna ttabauuhum bi ihsanin – na
lladhiyna jaauw min baadihim
aakhariyna minhum lamma yal haku bihim – na
llahdhiyna tabauuhum bi ihsanin – na

No comments:

Post a Comment