Utangulizi
Qurani tukufu ni asili ya mwanzo ya utungaji wa sheria katika Uislam, na hii ni kwa sababu Qurani ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyomteremshia Mtume wake Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kupitia kwa Malaika Mwaminifu Jibril (Alayhi ssalaam).
Na yote yaliyomo ndani ya msahafu yanakubaliwa na Waislam wote kuwa ni yale yale aliyoteremshiwa Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) bila kubadilika chochote ndani yake, na husomwa katika Swala na katika hadhara nyingine kama ni ibada.
Qurani ni muujiza ambao Mwenyezi Mungu amewabishia makafiri kuleta mfano wake tangu miaka elfu moja mia nne na ishirini iliyopita na mpaka leo hii, baada ya kupita miaka yote hiyo, wameshindwa kuleta hata aya moja yenye mfano wake.
Kila kilichopokelewa kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kisichokuwa Qurani tukufu, katika yale yanayobainisha itikadi ya dini, yanayoisherehesha sheria, yanayohimiza kuyafuata maamrisho ya Qurani tukufu nk, yote hayo ni 'Sunnah', au huitwa 'Hadithi za Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)' au 'Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)'. Na yote hayo ni Wahyi aliofunuliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na Mola wake Subhanahu wa Taala.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pia hufanya Ijtihadi katika baadhi ya Hukmu, na Mwenyezi Mungu haithibitishi hukmu ya Ijtihadi iwapo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atakosea katika kujitahidi kwake, na hapo hapo atatumwa Malaika Jibril na kumsahihisha. Ama pale Mwenyezi Mungu anapoithibitisha Ijtihadi ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam), basi Ijitihadi hiyo huingia katika hukmu ya Sunnah, na kwa ajili hiyo Sunnah yote asili yake ni Wahyi.
Mifano ya Ijtihadi za Mtume wa Mwenyezi Mungu
Mateka wa Badar
Baada ya vita vya Badar kumalizika na Waislamu kurudi Madina na mateka wao, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliwataka shauri Sahaba zake juu ya mateka wa vita hivyo vya Badar.
Abubakar (Radhiya Llahu anhu) akamwambia:
"Mimi naona kuwa hawa ni jamaa zetu, kwa hivyo itakuwa bora kama tutachukua fidia kutoka kwao na pesa hizo sisi zitatusaidia katika mapambano yetu na makafiri, na wakati huo huo huenda Mwenyezi Mungu akawahidi hawa na kutusaidia siku za mbele."
Ama Umar (Radhiya Llahu anhu) akasema:
"Mimi sioni kama aonavyo Abubakar, bali naona itakuwa bora kama utanipa (jamaa yangu) 'fulani' nimkate kichwa chake, na Aly umpe (ndugu yake) Aqiyl amkate kichwa chake na Hamza umpe (jamaa yake) fulani amkate kichwa chake ili Mwenyezi Mungu ajuwe kuwa nyoyoni mwetu hamna mapenzi ya washirikina. Na hawa ni vigogo vya washirikina na viongozi wao."
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipendezewa na rai ya Abubakar (Radhiya Llahu anhu), akachukua fidia kutoka kwao na kuwaacha huru baadhi yao .
Usiku ule Jibril akateremsha aya kutoka kwa Mwenyezi Mungu Subahanahu wa Taala isemayo:
مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَى حَتَّى يُثْخِنَ فِي الأَرْضِ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا
وَاللّهُ يُرِيدُ الآخِرَةَ وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {67} لَّوْلاَ كِتَابٌ مِّنَ اللّهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ {68} فَكُلُواْ مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلاَلاً طَيِّباً وَاتَّقُواْ اللّهَ إِنَّ اللّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ {69}
"Haimpasi Nabii kuwa na mateka mpaka apigane (sana) na kushinda (barabara) katika nchi (ndipo achukue mateka). Mnataka vitu vya dunia, hali Mwenyezi Mungu anataka Akhera! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, (na) Mwenye hikima.
Isingalikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu (kuwa Mwenye kujitahidi mwisho wa jitihada yake hateswi) bila shaka ingalikupateni adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.
Basi kuleni katika vile mlivyoteka (vitani), ni halali (yenu sasa) na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu."
Al Anfal - 67 - 69
Isipokuwa deni
Imepokelewa kutoka kwa Abu Qatada (Radhiya Llahu anhu) kuwa siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipokuwa juu ya membari yake akihutubia, mtu mmoja alisogea mbele akauliza:
"Iwapo nitauliwa katika jihadi nikiwa nimesubiri nikitegemea malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu huku nikiwa nakwenda mbele na sirudi nyuma, Mwenyezi Mungu atanisamehe madhambi yangu yote?"
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamjibu:
"Ndiyo, utasamehewa".
Yule mtu alipoondoka, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaamrisha aitwe, na alipokuja akamwambia:
"Ndiyo utasamehewa, isipokuwa deni, hivi ndivyo alivyonambia Jibril alayhi ssalaam (hivi punde)".
Annasai
Kuwapiga wake wanaopindukia katika kuasi
Imepokelewa kutoka kwa Ibni Jariyr na Ibni Mardaweya kuwa Al Hassan al Basry amesema:
"Mwanamke mmoja alikwenda kushitaki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa amepigwa na mumewe usoni akafanya alama.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:
"Lazima na yeye (mwanamke) alipe kisasi chake".
Mwenyezi Mungu akateremsha aya ya 34 ya Suratul Nisaa isemayo:
الرجال قوامون على النساء بما فضل الله بعضهم على بعض وبما أنفقوا من أموالهم فالصالحات قانتات حافظات للغيب بما حفظ الله واللاتي تخافون نشوزهن فعظوهن واهجروهن في المضاجع واضربوهن فإن أطعنكم فلا تبغوا عليهن سبيلا إن الله كان عليا كبيرا.
"Wanaume ni walinzi wa wanawake kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine, na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii wanaojihifadhi (hata) wasipokuwapo (waume zao) kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha wajihifadhi. Na wanawake ambao mnaona uasi wao kwenu, waonyeni na waacheni peke yao katika vitanda na wapigeni. Na kama wakikutiini msiwatafutie njia ya (ya kuwaudhi bure). Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye juu (na) Mkuu".
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:
"Nilitaka vingine lakini Mwenyezi Mungu ametaka kinyume chake'.
Dua ya Qunuti
Watu wa kijiji kimoja walimdanganya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa wamesilimu, na kwamba wanataka wapelekewe watu ili wawafundishe dini yao . Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akawapelekea watu sabini waliohifadhi Qurani. Lakini watu wa kijiji hicho waliwazungukia na kuwauwa wote.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akawa kila anaposwali, anapoinuka katika raka-a ya mwisho kutoka katika rukuu, anaposema 'Samia Llahu liman hamidah", alikuwa akisoma Qunuti na kuwalani watu wa kijiji kile cha wauaji kwa kusema:
"Allahumma mlaani fulani na fulani.."
Akawa anaendelea hivyo katika kila swala mpaka Jibril alipoteremsha aya kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kumtaka asiendele. Mwenyezi Mungu anasema:
لَيْسَ لَكَ مِنَ الأَمْرِ شَيْءٌ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ أَوْ يُعَذَّبَهُمْ فَإِنَّهُمْ ظَالِمُونَ
وَلِلّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ يَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ
وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ
"Wewe huna lako katika shauri hii - au (Mwenyezi Mungu) awaonee huruma au awaadhibu, maana wao ni madhalimu (Atafanya anavyoona mwenyewe).
Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini humsamehe amtakaye na kumwadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu".
Aali Imran - 128 - 129
Bukhari – Imam Ahmed na wengineo
Asili mbili
Qurani tukufu ni Wahyi. Unasomwa katika Swala na imepangiwa idadi ya thawabu katika kusoma kwake.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
من قرأ حرفا من كتاب الله فله به حسنة والحسنة بعشر أمثالها لا أقول الم حرف ولكن ألف حرف ولام حرف وميم حرف
Atakayesoma herufi katika kitabu cha Mwenyezi Mungu atapata kwa kila herufi moja thawabu, na thawabu moja kwa kumi za mfano wake. Sisemi Aliyf laam miym’ kuwa ni herufi (moja), bali aliyf ni herufi moja na laam ni herufi moja na miym ni herufi moja
Lakini Sunnah ni Wahyi usiosomwa katika Swala, na si ibada katika kuisoma. Na zote mbili (Qurani na Sunnah) zinakwenda sambamba, kazi yake ni moja na wala hapana hitilafu baina yake. Zote hizo zinatufundisha yale Mola wetu anayoyataka kutoka kwetu. Ya kwanza (Qurani) inatoka moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu, na ya pili (Sunnah) inatoka kwa Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Yanayosadikisha haya ni kauli Yake Subhanahu wa Taala aliposema:
"Na tumekuteremshia mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, na ili wapate kufikiri".
An Nahl - 44
Na maana ya aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha mawaidha, nayo ni Qurani tukufu, ili Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) awabainishie watu yaliyomo ndani ya Qurani kutokana na elimu nyingine aliyopewa, nayo ni Sunnah yake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) iliyotwahirika.
Kwa hivyo Qurani ni asili ya mwanzo ya sheria ya Mwenyezi Mungu, na Sunnah ni asili ya pili.
Kwa hivyo Qurani na Sunnah ni asili mbili zinazoambatana, zisizohitilafiana katika kutimiza sheria ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa taala, na Muislam hawezi kuijuwa sheria ya Mwenyezi Mungu bila ya mojawapo ya asili mbili hizi. Na Mwanachuoni yeyote au hata mwenye kufanya Ijtihadi hana budi kutafuta hoja zake kutoka katika asili mbili hizi.
Anasema Ibni l Qayim Al Jawziy:
"Mwenyezi Mungu anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَطِيعُواْ اللّهَ وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُوْلِي الأَمْرِ مِنكُمْ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللّهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ ذَلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلاً (59)
"Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema."
AnNisaa - 59
Mwenye kuichunguza aya hii ataona kuwa Mwenyezi Mungu anatuamrisha kumtii Yeye na kumtii Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa ukamilifu. Bimaana kuwa iwapo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atatuamrisha au kutukataza jambo, basi inatuwajibikia kumtii kwa ukamilifu hata kama amri hiyo haimo ndani ya Qurani, kwani yeye (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kama alivyosema katika hadithi:
ألا أني أوتيت هذا الكتاب ومثله معه"
"Hakika mimi nimepewa hiki Kitabu na (nimepewa) nyingine yenye mfano wake pamoja nayo". (Nayo ni Sunnah yake)".
Abu Daud na ImamMalik katika Muwata’a
Ukiichunguza tena aya ya Annisaa -59 utaona kuwa Mwenyezi Mungu hakutuamrisha kumfuata mwenye madaraka moja kwa moja kama alivyotuamrisha kumfuata Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Bali Mwenyezi Mungu amesema:
"Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume"
Na hakusema "Mtiini wenye madaraka katika nyinyi", bali amesema:
"Na wenye madaraka katika nyinyi" – bila kuingiza neno 'Mtiini' kama ilivyo katika twa- a Yake na ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Kwa ajili hiyo, ili mwenye madaraka atiiwe lazima amri yake ikubaliane na maamrisho ya Mwenyezi Mungu au ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Na kama amri ya mwenye madaraka itakwenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam), basi hapana utiifu katika kumuasi Muumbaji.
(Mwisho wa maneno ya Ibnul Jawzi).
Kisha Mwenyezi Mungu akaikamilisha aya hiyo kwa kusema:
"Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume".
Kauli hii inatujulisha kwa uwazi kabisa kuwa marejeo yetu sisi Waislam katika
kuhukumu ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Aina za Sunnah
Katika kamusi la Fiq-hi, neno 'Sunnah', maana yake ni; 'kila kilichothibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa Amekitamka, Amekitenda au Amekikubali.
Na mfano wake ni kama ifuatavyo;
1. Aliyotamka; Ni yale maneno aliyotamka katika matukio mbali mbali yanayohusiana na Itikadi, Adabu na mengineyo. Kwa mfano kauli yake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pale aliposema:
إنما الأعمال بالنيات
"Hakika ya matendo hufuatana na nia"
Au aliposema:
لا ضرر ولا ضرار
"Hairuhusiwi kudhuru wala kujidhuru"
2- Aliyotenda; Nayo ni yale matendo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) tuliyojulishwa na Masahaba (Radhiya Llahu anhu), kama vile namna alivyokuwa Akitawadha, Akiswali Akihiji nk.
3- Aliyoyakubali; Ni zile kauli au matendo waliyokuwa wakitamka na kutenda Masahaba (Radhiya Llahu anhum) mbele yake, na yeye (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akayakubali au akayanyamazia ikiwa ni dalili kuwa ameridhika nayo.
Na mfano wake unapatikana katika hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Annasai na kusimuliwa na Abu Saeed al Khudhary (Radhiya Llahu anhu) kuwa;
Watu wawili waliokuwa safarini uliwafikia wakati wa swala na hawakupata maji, wakatayammam na kuswali. Baada ya kuswali wakapata maji. Mmoja wao akatawadha na kuswali tena, lakini mwenzake hakurudia kuswali. Waliporudi kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kumuuliza juu ya hukmu yao, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema kumwambia yule asiyerudia kuswali; "Wewe umeisibu Sunnah sawa sawa", na akamwambia yule aliyerudia; "Wewe umepata thawabu mara mbili".
Dalili ya kuwajibika kuifuata Sunnah
Baadhi ya watu wanaojinasibisha na Uislam wamejaribu kuishambulia Sunnah - (Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa hoja mbali mbali. Wapo miongoni mwao wanaoikataa moja kwa moja, na wengine wanazikataa baadhi ya Hadithi, hasa zile ambazo katika elimu ya Hadithi zinazoitwa Hadithi za Aahad, na wapo wanaozikataa hadithi za aina hiyo zile tu zinazozungumzia mambo ya Itikadi nk.
Wale wanaokataa moja kwa moja kuwajibika kufuata Sunnah za Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni watu wenye kusudi la kutaka kuifasiri Qurani kwa namna waitakayo wao, kwa sababu Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ndiyo yanayotufasiria Qurani na kutubainishia. Ikiwa watafanikiwa kuipiga vita Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), basi itakuwa wepesi kwao kuipiga vita Qurani Tukufu kwa kuzitumia zile aya zinazobeba maana nyingi (Mutashabihaat) na zile hukmu zilizoachiwa huru (Mutlaq), kwani wao wataweza kuzibebesha hukmu hizo maana wanayotaka, na si kwa maana anayotaka Mola wetu Subhanahu wa Taala. Kwa sababu katika Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pana vizuizi vinavyozuwia mtu asiweze kucheza na maana ya Aya.
Jambo linaloshangaza ni kwamba hao wanaoipinga Sunnah ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) eti wanajiita 'Al Qur-aniyyun' (wenye kuifuata Qurani tu), wakati anayechunguza hali zao ataona kuwa kujinasibisha kwao huko na Qurani ni uongo mtupu, kwa sababu kwa kupinga kwao Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wao wanakwenda kinyume na mafundisho ya Qurani Tukufu.
Kwa sababu katika Qurani Mwenyezi Mungu anasema:
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُو
"Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho".
Al Hashar - 7
Na anasema:
وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْراً أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالاً مُّبِيناً
"Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanapokata shauri wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hakika amepotea upotofu (upotevu) ulio wazi (kabisa)".
Al Ahzab - 36
Baadhi ya dalili za kuwajibika kufuata mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
A – Dalili katika nguzo za Imani
Katika shuruti za Imani, ni kuyakubali yote aliyokuja nayo Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam), kwa sababu Mwenyezi Mungu amemchagua na kumwaminisha Mtume huyu mtukufu atufikishie maamrisho Yake kwetu.
Na Mwenyezi Mungu anasema:
{واللّه أعلم حيث يجعل رسالته}
"Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake."
Al An-an-am124
Na akasema:
فَهَلْ عَلَى الرُّسُلِ إِلاَّ الْبَلاغُ الْمُبِينُ
"Basi lipo lolote juu ya Mitume isipo kuwa kubalighisha kwa uwazi?"
An Nahl - 35
Na akasema:
} يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ آمِنُواْ بِاللّهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَى رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِيَ أَنزَلَ مِن قَبْلُ وَمَن يَكْفُرْ بِاللّهِ وَمَلاَئِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ
ضَلاَلاً بَعِيداً}
"Enyi mlio amini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha kabla yake. Na anaye mkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha potelea mbali."
AnNisaa - 136
Na akasema:
فَآمِنُواْ بِاللّهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللّهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ
"Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka".
Al Aaraf - 158
Hizi ni dalili zilizo wazi zinazotuamrisha kufuata mafundisho ya Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Anasema Imam Shafi Rahimahu Llah:
"Mwenyezi Mungu amejaalia ukamilifu wa Imani katika kumuamini Yeye kisha katika kumuamini Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam)."
Kitabul Umm
B – Dalili za kutii katika Qurani tukufu
Katika Qurani tukufu mna aya nyingi zinazoelezea juu ya kuwajibika kuti na kufuata Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Mwenyezi Mungu anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَطِيعُواْ اللّهَ وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُوْلِي الأَمْرِ مِنكُمْ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللّهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ ذَلِكَ خَيْرٌ َأَحْسَنُ تَأْوِيلاً
"Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema."
An Nisaa - 59
Kumtii Mwenyezi Mungu ni kukifuata kitabu Chake, na kumtii Mtume ni kufuata mafudisho yake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Mwenyezi Mungu pia amesema:
وما آتاكم الرسول فخذوه وما نهاكم عنه فانتهوا
"Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho".
Al Hashar - 7
Na katika aya ifuatayo, Mwenyezi Mungu ameliweka wazi kabisa kusudi Lake, pale aliposema:
فَلاَ وَرَبِّكَ لاَ يُؤْمِنُونَ حَتَّىَ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لاَ يَجِدُواْ فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجاً مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيماً
"La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye WEWE ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenykee kabisa ".
An Nisaa - 65
C – Dalili katika mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
تركت فيكم أمرين لن تضلوا ما تمسكتم بهما كتاب اللّه وسنتي
"Nimekuachieni amri mbili hamtopotea mkizishika; Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah yangu (Mafundisho yangu)".
Imam Malik - Al Hakim
Na akasema:
عليكم بسنتي وسنة الخلفاء الراشدين عضوا عليها بالنواجذ
"Mzifuate Sunnah zangu na (Sunnah) za Makhalifa waongofu, mzikamate vizuri kwa magego yenu".
Sunan Abu Daud
Hadithi hizi ni dalili kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amepewa Kitabu na Sunnah, na kwamba inatuwajibikia kuvifuata na kuvikamata vizuri, kuvitii na kuvifanyia kazi vyote viwili bila ya kuvitenganisha.
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ametutahadharisha juu wale watakaokuja baada yake watakaokataa kufuata mafundisho yake wakidai kuwa eti Qurani peke yake inatosha.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
يُوشِكُ الرَّجُلُ مُتَّكِئًا عَلَى أَرِيكَتِهِ يُحَدَّثُ بِحَدِيثٍ مِنْ حَدِيثِي فَيَقُولُ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ كِتَابُ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ مَا وَجَدْنَا فِيهِ مِنْ حَلَالٍ اسْتَحْلَلْنَاهُ وَمَا وَجَدْنَا فِيهِ مِنْ حَرَامٍ حَرَّمْنَاهُ أَلَّا وَإِنَّ مَا حَرَّمَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مِثْلُ مَا حَرَّمَ اللَّهُ "
"Hivi karibuni (mtaona ya kushangaza) utamkuta mtu ameegemea tandiko lake, anahadithiwa Hadithi katika hadithi zangu, anasema: "Baina yetu na baina yenu ni kitabu cha Mwenyezi Mungu (peke yake), tutakayoyaona yamehalalishwa ndani yake tutayahalalisha na tutakayoyaona yameharamishwa ndani yake tutayaharamisha" - Mjuwe kuwa yaliyoharamishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni sawa na yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu".
Ibni Majah - Al Baihaqiy - Abu Daud.
Na katika hadithi nyingine, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
مَن بلغه عني حديث, فكذب به, فقد كذب ثلاثة: الله, ورسوله , والذي حدث به
"Mtu atakapojulishwa juu ya hadithi yangu akaikadhibisha, (basi) amekadhibisha watatu. Mwenyezi Mungu, Mtume wake na yule aliyemfikishia hadithi hiyo".
Attabarani
Bila shaka hapa panakusudiwa zile hadithi sahihi
D – Dalili za Ijma'a
Umma wote wa Kiislam kwa ujumla umekubaliana juu ya kuwajibika kuifanyia kazi Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) katika sheria ya Mwenyezi Mungu, na hii inatokana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) yanayotutaka tuisimamishe hukmu ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata Kitabu Chake na Mafundisho ya Mtume Wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam), kwa sababu hizi ni asili mbili za sheria kwa Umma wa Kiislam, asili ambazo Mwenyezi Mungu ametujulisha nazo na kushuhudia Mwenyewe kuwa Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hasemi isipokuwa yale aliyofunuliwa.
Mwenyezi Mungu anasema:
قُل لاَّ أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَآئِنُ اللّهِ وَلا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ إِنْ أَتَّبِعُ إِلاَّ مَا يُوحَى إِلَيَّ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الأَعْمَى وَالْبَصِيرُ أَفَلاَ تَتَفَكَّرُونَ {50}
"Sema; "Mimi sikwambieni kuwa ninazo khazina za Mwenyezi Mungu wala (sikwambieni kuwa) najua mambo ya siri (ya Mwenyezi Mungu). Wala sikwambieni kuwa Mimi ni Malaika. Mimi sifuati ila yale yaliyofunuliwa kwangu". Sema ; " Je, kipofu na mweye macho huwa sawa? Basi je, hamfikiri?"
Al An - am - 50
Kwa ajili ya yote haya Waislam wakajifunza, wakailinda na kuifuata Sunnah ya Mtume wao (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kuiendeleza vizazi baada ya vizazi na wakaifanya kuwa ni marejeo yao katika mambo yote ya dini yao na kuifanyia kazi pamoja na kuikamata sawa sawa na kuihifadhi ili wawe wafuasi wa kweli wa Mtume wao Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Baadhi ya mifano ya umma kushikamana na mafundisho ya Mtume wao (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
1- Mtu mmoja alimuambia Abdillahi bin Omar (Radhiya Llahu anhu):
"Katika Qurani hatuoni maelezo yoyote juu ya Swala ya safari (Swalatu Ssafar).
Akajibu (Radhiya Llahu anhu):
"Mwenyezi Mungu alipotuletea Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) sisi hatukuwa tukijuwa lolote, kwa ajili hiyo tunatenda yale tuliyokuwa tukimuona Muhammad akitenda".
Na katika riwaya nyingine:
"Tulikuwa tumepotoka, Mwenyezi Mungu akatuongoza kupitia kwa Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam)".
Imam Ahmad
2- Mwanamke mmoja alimwendea Abdillahi bin Masaood (Radhiya Llahu anhu) na kumwambia:
"Tumesikia kuwa unakataza kuunganisha nywele (kuvaa wigi nk.)".
Akasema:
"Ndiyo",
Akasema:
"(Makatazo hayo) Yamo katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu au ulipata kumsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Akajibu:
"Yamo katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na pia nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)".
Yule mwanamke akasema:
"Wallahi nimetafuta baina ya magamba ya msahafu (msahafu wote), na sikuyaona hayo unayoyasema".
Abdillahi bin Masaood (Radhiya Llahu anhu) akasema:
"Hujaona ndani yake mahali pameandikwa: "Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho?".
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا
Akasema:
"Naam - imeandikwa".
Akasema Abdillahi ibni Masaood (Radhiya Llahu anhu):
"Basi mimi nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akikataza kukata (au kuchuna) nyusi, kufanya mwanya (baina ya meno), kuunganisha nywele na kupiga chale (Tatoo) isipokuwa kwa ajili ya matibabu".
Imam Ahmed
Msimamo wa Sunnah mbele ya Qurani tukufu
Wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hapakuwa na asili nyingine ya kuhukumu isipokuwa Qurani na Sunnah. Kutoka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu walikuwa wakipata asili ya hukmu zote kwa ujumla, ingawaje mambo mengi hayakuweza kupatikana sharhi zake, isipokuwa katika yale yanayojulikana kwa uwazi kabisa, yale yasiyobadilika maana yake hata baada ya kupita muda mrefu. Haya ni katika mambo yanayohusiana na Itikadi, Ibada, hadithi za umma uliokuja kabla yetu, na mambo yanayohusiana na Tabia na Adabu kwa ujumla.
Lakini Sunnah ilikuwa ikikubaliana na Qurani, ikisherehesha yale yaliyoelezwa katika Qurani kwa ujumla, na kuyachambua yaliyotolewa hukumu kwa pamoja, ikifafanua yaliyoachwa wazi hukmu zake, na pia Sunnah ilikuwa ikitowa hukmu zisizotajwa katika Qurani bila ya kupingana nayo katika misingi yake, zikihakikisha kulifikia lengo lake. Na kwa ajili hiyo Sunnah ikawa inafanya kazi pamoja na Qurani bila ya matatizo yoyote.
Tumeona hapo mwanzo kuwa Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni sawa na Qurani tukufu tukichukulia kuwa zote hizo ni Wahyi, na kwamba zote hizo ni asili mbili za kuisimamisha sheria ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa heshima ya Qurani inaizidi heshima ya Sunnah kwa sababu kazi ya Sunnah ni kuisherehesha Qurani, na kwa kawaida kile kinachoshereheshwa, daraja lake huwa ni kubwa kuliko kile kinachosherehesha. Na mfano wake ni mfano wa tawi juu ya kigogo.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Na tumekuteremshia mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, na ili wapate kufikiri".
An Nahl - 44
Uhusiano wa Qurani tukufu na Sunnah upo namna nne
Pili - Sunnah inaisherehesha Qurani kama ifuatavyo;
1. Inayachambua yale ambayo Qurani imeyaelezea kwa ujumla; Sunnah inachambua yale yaliyoelezwa kwa ujumla yanayohusiana na Ibada na Hukmu. Kwa mfano; Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amebainisha nyakati za Swala, idadi ya Raka-a zake, namna ya kuswali, nguzo zake na hukmu zake, akasema:
صلوا كما رأيتموني أصلي
"Salini kama mnavyoniona nikisali"
Bukhari.
Wakati Qurani imetuamrisha kuswali tu, bila ya kutujulisha juu ya hukmu hizo.
Sunnah pia imesherehesha yale yaliyoelezwa kwa ujumla katika Qurani kuhusu Hija, na kuelezea juu ya hukmu zake, nguzo zake na fardhi zake pamoja na kutuwekea miqati (mipaka ya kuanzia na kumalizia) na kutujulisha juu ya siku zake nk. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:
خذوا عني مناسككم
"Chukueni kutoka kwangu ibada zenu."
Muslim.
Sunnah pia imetubainishia yale yanayowajibika katika Zaka, kiasi chake, nasabu yake, mambo ambayo Qurani imeyaelezea kwa ujumla tu, bila ya kuyasherehesha.
2. Sunnah pia inayahusisha yale yaliyotolewa hukmu za pamoja; Mfano wake ni yale aliyotubainishia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu pale aliposema:
يوصيكم الله في أولادكم للذكر مثل حظ الأنثيين
"Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu; mwanamume apate sawa na sehemu ya wanawake wawili."
An Nisaa- 11
Hii ni hukmu ya pamoja (Aam), katika kuwarithisha watoto mali za baba au mama zao, zikitujulisha kuwa kila mwana anarithi mali ya baba yake. Lakini Sunnah ikaja kutujulisha juu ya kuihusisha hukmu hii kwa watoto wote isipokuwa watoto wa Manabii, kwani Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
نحن معشر الأنبياء لا نورث
"Sisi Mitume haturithiwi - yale tuliyoacha ni Sadaka".
Fathi l Bari Uk. 289 Juzuu ya sita.
Na Sunnah pia ikaja kutujulisha kuwa watoto wote wanarithi isipokuwa aliyeuwa. (Iwapo mzee atauliwa na mwanawe).
Na hii inatokana na kauli yake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposema:
الْقَاتِلُ لاَ يَرِثُ
"Na muuwaji harithi".
Attirmidhiy na Ibni Majah
Mfano wa pili ni ile kauli ya Mwenyezi Mungu alipotuharamishia kula nyamafu na damu.
Mwenyezi Mungu anasema:
حرمت عليكم الميتة والدم ولحم الخنزير
"Mumeharimishiwa nyamafu na damu na nyama ya nguruwe.."
Al Maidah - 3
Juu ya kuwa aya hii inatukataza kula nyamafu, nayo ni mnyama aliyekwisha kufa bila kuwahiwa kuchinjwa kisheria, pamoja na kutukataza kunywa damu, lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ameturuhusu kula baadhi ya nyamafu na baadhi ya damu.
Katika hadithi Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
أُحلَّت لنا ميتتان ودمان، أما الميتتان فالسمك والجراد وأما الدمان فالكبد والطحال
"Tumehalalishiwa maiti mbili na damu mbili. Ama maiti mbili ni samaki na nzige ama damu mbili ni Maini na Bandama."
Ibni Majah - Imam Ahmed na Addaraqutny
3 Sunnah pia Inaiongoza hukmu iliyoachwa huru katika Qurani
Katika kauli yake Subhanahu wa Taala pale aliposema:
وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُواْ أَيْدِيَهُمَا جَزَاء بِمَا كَسَبَا
"Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke ikateni mikono yao; malipo ya yale waloyachuma."
Al Maidah - 38
Katika aya hii Mwenyezi Mungu hakuifunga hukmu yake kwa kuitaja sehemu gani ya mkono ikatwe. Wakati mkono (Yadun), katika lugha ya kiarabu hufasiriwa mpaka penye bega na wengine huufasiri mkono kuwa mpaka penye kisugudi na wengine mkono kwao ni kiganja tu, nk.
Lakini mwizi alipoletwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na baada ya kuthibiti wizi wake, akamkata penye kiganja chake.
Subuli ssalaam - Addaaraqutniy.
Tatu - Sunnah mara nyingine hutoa hukmu ikiwa kama ni tawi la hukmu iliyokwishatolewa katika Qurani ya kuhalalisha jambo, ikaja Sunnah kuiharamisha sehemu ya hukmu hiyo iwapo watu wataitumilia hukmu hiyo kwa ajili ya kuwaghilibu wenzao au iwapo itasababisha mapambano baina ya Waislam.
Na mfano wake ni pale Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipokataza kuuza mazao kabla ya mavuno, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) mara baada ya kuhamia Madina, aliwakuta wakulima wakiuziana mazao kabla ya kuanza kuonekana juu ya miti. Wanunuzi na wauzaji hawakuwa wakijuwa kiasi gani cha mazao kitakachopatikana. Unapofika wakati wa mavuno ndipo mshangao unapotokea, maana mara nyingi kwa ajili ya baridi kali au maradhi ya miti wanunuzi hao hula hasara baada ya kuharibika mazao, na kwa ajili hiyo mapambano makali hutokea baina yao . Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaharamisha uuzaji wa aina hii iwapo mazao bado hayajaonekana. Akasema:
"Mnaonaje Mwenyezi Mungu akizuwia yasipatikane mazao, mmoja wenu atakuwa amechukua mali ya mwenzake kwa ajili ya kitu gani?"
Fathu l Bari.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ametowa hukmu hiyo juu ya kuwa katika Qurani Mwenyezi Mungu ameruhusu kuuziana chochote iwapo watu wameridhiana wao kwa wao.
Mwenyezi Mungu anasema:
يا أيها الذين آمنوا لا تأكلوا أموالكم بينكم بالباطل إلا أن تكون تجارة عن تراض منكم
"Enyi mlioamini! Msiliane mali zenu kwa batili. Isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu ( hiyo inajuzu)…"
An Nisaa - 29
Nne - Sunnah pia inaweza kutoa hukmu ya peke yake ya kuharamisha, juu ya kuwa Qurani haikufanya hivyo.
Kwa mfano; Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipoharamisha kula nyama ya punda, wanyama wenye meno wanaokula watu nk., ambao hadithi zake ni nyingi na zimekuja wazi katika Bukhari - Muslim - Abu Daud Annasai na wengineo, ingawaje katika Qurani nyama hizo hazikuharamishwa.
Mwenyezi Mungu anasema:
قل لا أجد فيما أوحى إليّ محرما على طاعم يطعمه إلا أن يكون ميتة أو دما مسفوحا
"Sema; "Sioni katika yale niliyofunuliwa kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni mzoga au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe…"
Al An-am - 145
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pia ameharamisha mtu kuoa Ammati ya mkewe au Khale yake akawachanganya pamoja, juu ya kuwa katika Qurani hawakutajwa hao kuwa ni katika walioharamishwa. Kwani Mwenyezi Mungu baada ya kutujulisha juu ya wale walioharamishwa kuolewa akasema:
وأحل لكم ما وراء ذلك
"Na mmehalalishiwa (kuoa wanawake) minghairi ya hawa".
An Nisaa - 24
Yote haya ingawaje hayakutajwa katika Qurani, lakini yamekuja kuharamishwa katika Sunnah na ni wajibu kwetu kuyafuata na kusema Sam-an wa Taa-an.
Marejeo;
Nahwa thaqafa Islamia asiylah - Dr. Omar Suleiman Al Ashqar
Mukhtasar wajiyz fiy Ulum l Hadith - Dr. Muhammad Ajjaj Al Khatib
Al Umm - Imam Shafi
Tafisiri ya Ibni Kathir
Tafsiri ya Sh. Abdullah Saleh Farsy
Tafsiri ya Sh. Ali Muhsin
Al Rahiqul Makhtum - Sheikh Safiurahman Al Mubarakfurri
Haadha l Habiyb - Skheikh Abubakar Al Jazairiy
Fiq-hil Sunnah - Sayed Sabeq
No comments:
Post a Comment