Ndugu zangu Waislam
Assalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
Anasema Sheikh Yusuf Al Qaradhawi;
"Kuhalalisha au kuharamisha nyimbo, kwa kutumia ala za muziki au bila kutumia ala, ni suala lililokwishajadiliwa sana baina ya maulama tokea karne za mwanzo, wakakubaliana katika baadhi ya hukmu na kuhitalifiana katika baadhi nyingine.
Maulamaa wote (hata wale wachache sana wanaoona kuwa kuimba au kusikiliza nyimbo si haramu) wamekubaliana kuwa nyimbo yoyote ile yenye maneno yasiyokuwa na adabu ndani yake wala heshima, (yenye maneno machafu), au nyimbo zinazohimiza watu katika kufanya maasi na uovu ni haramu, na hii ni kwa sababu nyimbo ni maneno, na maneno mazuri ni halali na maneno mabaya ni haramu.
Kwa vile kila kauli inayokwenda kinyume na mafundisho ya kiislam ni haramu, basi bila shaka maneno mabaya yanayotamkwa ndani ya nyimbo na kusikilizwa na watu wengi, yakichanganyika na ala za muziki, jambo linaloongeza kuleta taathira, bila shaka haramu yake ni kubwa zaidi. Kwa vyovyote vile maneno maovu ni haramu hata kama yatatamkwa kwa sauti ndogo ya kusikiwa na msemaji peke yake bila mtu mwingine kusikia.
Wakakubaliana maulamaa wote pia juu ya uhalali wa kuimba kwa maneno mema (bila ya kutumia ala, isipokuwa 'vitari' - 'virika') katika siku za furaha zilizowekewa amri ndani yake katika dini, kama vile siku za sikukuuu, katika arusi au katika kumpokea mgeni aliyeondoka muda mrefu, jambo ambalo zipo amri zilizo wazi zinazoruhusu kufanya hivyo".
Wapo baadhi ya maulamaa wachache sana waliojuzisha nyimbo za aina hiyo yote sawa ikiwa kwa kutumia ala za muziki au bila kutumia ala".
(Mwisho wa maneno ya Al Qaradhawi).
AYA ZINAZOHARAMISHA MUZIKI
Katika Suratul Najm - aya ya 60 mpaka 62, Mwenyezi Mungu anasema;
"Afamin hadha l hadithi taajabun".
(Mnaistaajabia hadithi hii?)
"Wa tadh-hakuna wala tabkun".
(Na mnacheka; wala hamlii?)
"Wa antum SAMIDUN".
(Na mmeghafilika (muko ndani ya starehe zenu) tu!?).
Katika kuifasiri aya hii anasema Mwanachuoni maarufu Imam Al Tabari;
"Kauli ya Mwenyezi Mungu pale alipouliza; 'Mnaistaajabia hadithi hii?' - maana yake ni Qurani). Yaani badala ya kulia kutokana na yanayotajwa ndani ya Qurani katika adhabu za siku ya Kiama na mengineyo, nyinyi mnakanusha na kuendelea na starehe zenu?".
'Na mnacheka wala hamlii?', kwa hofu na kwa kuiogopa siku ya Kiama?
'Wa antum samidun?'. Maana yake 'Mumezama katika starehe na nyimbo?'.
Anasema mwanachuoni huyo kuwa; Katika lugha ya ki Hamyar, (watu wa Yemen), neno 'Samada' maana yake ameimba. Walikuwa wakitaka kumwambia mtu awaimbie, wakimwambia; 'Samid lana', yaani 'tuimbie', au wakimwambia mwanamke; 'Ismidina', yaani (Tustareheshe kwa kutuimbia)."
Mwisho wa maneno ya Al Tabari
MANENO YA UPUZI
Mwenyezi Mungu anasema;
"Na katika watu wanaokhitari maneno ya upuzi (lahwal hadiythi) ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo wao kujua lolote…"
Luqman - 6
Katika kuifasiri aya hii mwanachuoni maarufu Imam Al Sayutiy katika kitabu chake kiitwacho 'Al Mandhur fiy tafseer al Maathur' anasema;
"Amesema Al Baihaqy kuwa neno 'Lahwal hadiythi' lililotumika katika aya hii maana yake ni; 'maneno yaliyo batili'..
Na alipoulizwa Ibni Abbas (RA) juu ya maana ya neno 'Lahwal hadiythi', akasema;
'Maneno yasiyokuwa ya kweli, nayo ni nyimbo na yaliyo mfano wake'.
Bukhari, Al Bayhaqi kutoka kwa Ibni Abi Duniya.
Katika hadithi nyingine iliyotolewa na Ibni Abi Duniya na kusahihishwa na Al Baihaqiy, kutoka kwa Abi Ssaha-baa amesema;
"Nilimuuliza Abdillahi ibni Masaud (RA) juu ya tafsiri ya kauli ya Mwenyezi Mungu (Lahwal hadiythi) 'maneno ya upuzi', akasema;
"Naapa kwa yule ambaye hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye kuwa, (maneno hayo) ni nyimbo".
Kutoka kwa Ibni Abi Dunia pia na Ibni Jarir kuwa alipoulizwa Ikrima (RA) juu ya maana ya neno (lahwal hadiythi) akasema;
"Ni nyimbo".
Anasema Sheikh Al Qaradhawi;
"Kusikiliza maneno ya upuzi, hukmu yake inaweza kuwa makruh na kwamba si lazima iwe haramu, hii ikiwa hamna ndani yake kuwasengenya watu, kuwabughudhi, matusi na maneno yasiyokuwa na heshima na yasiyokuwa na adabu".
ATHARI ZA NYIMBO
Imepokelewa kutoka kwa Ibni Masaud (RA) pia kuwa Mtume (SAW) amesema;
"Nyimbo inamea unafiki katika nyoyo kama miti inavyomea kwa maji".
Al Baihaqi.
Alipoulizwa Al Qasim bin Muhammad (RA) juu ya nyimbo iwapo ni haramu au halali akajibu;
"Nambie ewe mwana wa ndugu yangu! Siku ile Mwenyezi Mungu atakapoiweka batili yote upande mmoja, na haki yote upande mmoja, unadhani nyimbo zitawekwa upande gani?"
Ibni Abi Dunia
SAUTI MBILI ZILIZOLAANIWA
Mtume (SAW) amesema;
"Sauti mbili zimelaaniwa duniani na akhera, mzumari (unaopigwa) kwa ajili ya neema na kilio (mtu akilia kwa kupiga kelele na kuomboleza) katika msiba".
Bukhari na Attirmidhiy
Katika kuifasiri hadithi hii, mmoja katika wanavyouni wa kiislam aitwae Al Khutab amesema;
"Hii ni dalili kuwa katika nyakati zisizokuwa hizo, tunaruhusiwa kuimba". Lakini wanachuoni wakubwa kama vile Al Qurtubiy na Ibni Taimia wamesema;
"Bali hii ni dalili ya kuharimishwa kwake".
Kauli hii ya mwisho ndiyo yenye uzito zaidi, kwa sababu Mtume (SAW), anatukataza kuyafanya hayo pale mtu anaponeemeshwa na badala yake anatakiwa amkumbuke Mola wake na kumshukuru, basi anapopatwa na masaibu au misiba anatakiwa amkumbuke zaidi, kwa sababu katika kumtaja Mwenyezi Mungu moyo unapata matumaini.
Kwa vyovyote vile Muislam anatakiwa awe daima anajishughulisha na kumdhukuru Mola wake pamoja na kusoma maneno yake badala ya kujishughulisha na kusikiliza maneno ya upuzi yasiyomridhisha Mola wake.
Katika hadithi nyingine Mtume (SAW) amesema;
"Watakuja kutokea watu katika umati wangu watakaohalalisha kuzini na hariri na ulevi na ala za muziki…"
Bukhari
Kauli ya Mtume (SAW) hapa inaleta maana kuwa yote hayo ni haramu, na kwamba watakuja watu katika umati wake watakaoyahalalisha. Kwa hivyo unapowasikia watu wakihalalisha mambo hayo, juwa ya kuwa hiyo ni mojawapo ya ushahidi kuwa Mtume Muhammad (SAW) ni Mtume wa kweli, kwa sababu yale aliyotuambia kuwa yatakuja kutokea katika kuhalalisha yaliyoharamishwa yametokea kweli
Imesimuliwa na Attirmidhiy kuwa Ali bin Abi Talib (RA) amesema kuwa Mtume (SAW) alimwambia;
"Umati wangu ukijishughulisha na kufanya mambo kumi na tano (yafuatayo), basi itakuwa halali kwao kupatwa na balaa…", akataja waimbaji na ala za muziki kuwa ni miongoni mwa mambo hayo kumi na tano.
Katika aya zilizotangulia pamoja na hadtihi za Mtume (SAW) tumeona namna gani Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anavyochukizwa na maneno ya upuzi na yasiyokuwa na heshima, na tumeona pia namna gani Mtume (SAW) anavyochukizwa na maneno ya namna hiyo. Bila shaka kuchukizwa huko kunakuwa kukubwa zaidi pale maneno hayo yanapochanganyika na sauti za ala za muziki, jambo ambalo Mtume (SAW) keshavitaja kuwa miongoni mwa mambo yanayompeleka mtu kupata laana ya Mwenyezi Mungu, na kumpatia ghadhabu zake Subhanahu wa taala.
Bila shaka penye Nyimbo na ala za Muziki, hasa zile nyimbo zinazoingiza matamanio maovu nyoyoni, kwani katika nyimbo za siku hizi ni nadra kusikia nyimbo zisizokuwa na maneno ya aina hiyo.
Kwa hivyo katika hadhara za namna hiyo mara nyingi unakuwepo mchanganyiko wa wanawake na wanaume, na hii husababisha uhusiano maalum baina ya pande mbili hizo, ama sivyo kwa nini basi tunaona mwimbaji anapokuwa mwanamke, basi mtunzaji anakuwa mwanamume na kinyume cha hivyo pale anapoimba mwanamume anayetunza ni mwanamke?
Au kwa nini kila anapokufa mwimbaji maarufu wa kiume utasikia wanojiuwa kwa masikitiko ni wanawake na wanapokufa waimbaji wanawake wanaojiuwa ni wanaume?
Kwa ajili hii maulamaa wakasema;
"Nyimbo yoyote ile yenye kutaja wanawake na kuwasifia uzuri wao na sehemu zao za mwili, nyimbo zenye kuzungumza juu ya uhusiano wa mwanamke na mwanamume nje ya ndoa, au zile zinazotaja ulevi na yaliyoharamishwa kwa kuyasifia, yote hayo hapana hitilafu yoyote ile baina ya maulamaa kuwa ni haramu.
Ama zile nyimbo zisizokuwa na hayo na ikiwa zinaimbwa katika wakati mdogo sana, tena katika siku za furaha tu na arusi au katika sikukuuu au kwa ajili ya kuwachangamsha watu katika kazi ngumu, tena bila ya ala za muziki kama ilivyokuwa wakati lilipokuwa likichimbwa handaki katika vita vya Ahzab, pale Masahaba (RA) walipokwakiimba;
"Wallau kama si Mwenyezi Mungu tusingeongoka
Wala tusingetoa sadaka wala tusingesali
Akatuteremshia utulivu juu yetu
Na kuithibitisha miguu yetu".
Nyimbo za mfano huu hapana hitilafu yoyote ile baina ya maulamaa kuwa si haramu.
Baadhi ya maulamaa wakasema kuwa hapana neno ikiwa itatumiwa ngoma wakati wa vita tu, kwa sababu wanasema kuwa ngoma inaingiza hofu ndani ya nyoyo za adui. Ama kupiga vitari, maulamaa wote wamekubaliana kuwa si haramu, kwa sababu Mtume (SAW) aliimbiwa na alipigiwa vitari alipoingia mji wa Madina, na Abubakar (RA) alipotaka kuwakataza waliokuwa wakimpigia Mtume vitari hivyo, Mtume (SAW) akamwambia;
"Waache Abubakar, ili Mayahudi wapate kujuwa kuwa dini yetu ni nyepesi".
Zipo pia hadithi zinazosema kuwa Mtume (SAW) aliamrisha vitari vipigwe katika arusi.
Vyote hivyo ni halali ikiwa vitaambatana na nyimbo zenye maneno mema.
Alipoulizwa Sheikh Ibnul Baaz kuhusu kusikiliza nyimbo kama ni halali au haramu akajibu;
"Kusikiliza nyimbo ni haramu na ni katika sababu kubwa zinazoleta maradhi ya nyoyo".
Kisha akaisoma ile aya iliyotanguliwa kutajwa hapo juu (Wamina nnasi man yashtari lahwa l hadiythi…), akasema kuwa Ibni Masaud (RA) aliifasiri aya hiyo kuwa maana yake ni Nyimbo. Na Mtume (SAW) alisema; "Watakuja kutokea watu katika umati wangu watakaohalalisha kuzini na kuvaa nguo za hariri na ulevi na ala za muziki…", kwa hivyo nakuusia usijishughulishe na kusikiliza nyimbo na badala yake jishughulishe na kusikiliza idhaa ya Qurani tukufu, kwani ndani yake mna manufaa mengi sana.
Ama katika arusi, inaruhusiwa kupiga virika (vitari) na kuimba nyimbo ya kawaida isiyokuwa na maneno ya kuwaita watu katika kumuasi Mwenyezi Mungu wala katika yale yaliyoharamishwa na hii ni kwa sababu Mtume (SAW) aliruhusu hivyo. Ama kupiga ngoma, hiyo haijuzu".
(Mwisho wa maneno ya Ibni l Baaz).
MTUME (SAW) ALIRUHUSU NYIMBO KATIKA SIKU YA SIKU KUU
Bibi Aisha (RA) amesema;
"Siku moja Mtume (SAW) aliingia chumbani kwangu akawakuta vijana wawili wa kike wakiimba nyimbo za vita, akaegemea tandiko na kuugeuza uso wake upande mwingine (na katika riwaya nyingine - Akaufunika uso wake). Akaingia (baba yangu) Abubakar (RA) na kunikataza, akasema; 'Mizumari ya shetani katika nyumba ya Mtume (SAW)?" Mtume (SAW) akamwambia;
"Waache".
Na katika riwaya nyingine alimwambie;
"Waache kwa sababu kila watu wana siku kuu zao"
Mtume (SAW) alipokuwa akiangalia upande mwingine (Abubakar (RA)) akawatizama kwa macho makali, wakaondoka.
Bukhari na Muslim
Tanbih;
a- Neno zumari hapa halina maana ya lile zumari linalopulizwa, bali maana yake ni nyimbo au mashairi.
b- Wanawake hao walikuwa wakiimba nyimbo za vita
Imetolewa na Bukhari pia kuwa Bibi Aisha (RA) aliwahi kuachiliwa na Mtume (SAW) kutizama ngoma ya Wahabeshi waliokuwa wakicheza kwa mikuki na ngao ndani ya uwanja wa msikiti.
NIMEWATUMIA UJUMBE ILI NANYI MUUTUME.
WAILAAHUNA SALAM ALAYKUM.
No comments:
Post a Comment