بسم الله الرحمن الرحيم


بسم الله الرحمن الرحيم

UDOMSA.

Monday, 20 September 2010

MAONYO NDUGU ZANGU

Assalamu alaykum

Bismillahi Rrahmaani Rrahiim



Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema:

“Nifikishieni ujumbe wangu japo kwa aya moja.”



Uislamu umemharamishia mwanamke kuvaa nguo zenye kudhihirisha na kuonyesha viungo vya ndani vya mwili wake na vile vile zile zenye kubana na kudhihirika umbo lake, khasa zile sehemu zinawavutia watu kama maziwa (matiti), kiuno, matako na kadhalika.



Mambo kama haya ni mabaya sana kwani imesimuliwa katika hadithi sahihi kuwa;

Abu Huraira amesema: Mtume (s.a.w) amesema:

“Watu wa namna mbili katika watu wa motoni sijawaona;

Watu wenye mijeledi (viboko) kama mikia ya ngombe wanawapiga watu (ishara juu ya wale viongozi madhalimu maadui wa watu), na wanawake wavao nguo kama wasiovaa kitu (wako uchi, wanawafundisha wenziwao kufanya kama wao), wakenda hujiringisha na kujikatishakatisha (kiuno, khasa kutikisa matako kwani ndio vutio ya wale wenye maradhi ya uchafu) na vichwa vyao kama nundu za ngamia zilizoinama,hawaingii Peponi wala kusikia harufu yake juu ya kuwa harufu yake itasikika umbali wa masafa kadha wa kadha).”

Hadith



Maelezo ya hadith:

1.Wanawake hawa wametajwa kuwa ni wenye nguo kwa sababu watakuwa wanavaa nguo lakini zisizokuwa na sitara yoyote kwa wepesi wake, na kuonya kwake zikawa zitaonyesha vyote vya ndani kama yalivyo mavazi ya wanawake wetu wa leo wendao uchi (yaani wanavaa nguo lakini kama hawakuvaa), kila kitu kinaonyesha, alama za mavazi ya ndani na kifua wazi, na kusimamisha matiti na kadhalika, na kisha ndio unaambiwa ni dunia ya leo; Dunia ya leo? Basi jiandae na kuwa kuni ya moto wa Jahannam pindi ukijifanya mkaidi na makatazo ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w), na Mwenyezi Mungu atuepushie na moto huo na ndugu zetu wakike wa kiislamu (amin), kwani wao ndio waliotajwa kuwa ndio wengi huko motoni na hii ni pale Mtume (S.A.W) alipokwenda safari ya Miiraj na kuoneshwa hao (wanawake wa umma wake) motoni.



2. Kadhalika vichwa vyao vimesifiwa kuwa ni kama manundu ya ngamia kwa vile namna wanavyoziinua nywele zao na kuzifunga kati ya kichwa, kama kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akipiga mfano wa hawa wanawake wa siku hizi wanaokwenda sehemu maalum kwa ajili ya kunyoshwa nywele zao na kutengenezwa na kufanya mitindo hii na ile, na utakuta wanowatengeneza hivyo ni wanaume (la haula walaanifu wakubwa, tena mabaradhuli) na kazi zote za ulaanisi.



Mtume (s.a.w) amesema:

“Amewalani Mwenyezi Mungu wanawake wanaojifananiza na wanaume, na wanaume wanaojifananiza na wanawake.”

Na hili ni jambo baya sana lililoenea ulimwengu wetu wa kiislamu, khasa huko nyumbani imekuwa ndio mtindo, kwani imefikia hata kuwapo eti maharusi wakioana wanaume kwa wanaume na haya yameshuhudika mwaka juzi huko nyumbani katika moja ya pwani za kitalii nao ati ni Waislamu.

Na pia kuoana wanawake kwa wanawake pia huko nyumbani na haya mambo yanaendelezwa.

Mambo ni khatari sana kwani ni kinyume na maumbile ambayo Mungu amewaumbia, na kinyume na maadili ya Kiislamu, na yanayotufika nyumbani sio kwa sababu ya walio kuwapo madarakani kwa kuwashambulia, lakini ni sisi wenyewe tumewacha mafunzo ya dini yetu, jee leo yasitufike hayo?



Na hawakutosheka na nyumbani, bali yamehamia huko ugenini walipo pia. Hakika habari tunozipata ni za kutisha, watu wavunjiana nyumba kimakusudi kwa kuchukuwa wake za watu, na katika mkasa uliotokea katika moja ya masherehe, wake wa watu wawili kutwangana ngumi mmoja wao akijidai anamchukulia mumewe. (Fa-atabiruu ya ulul absaar).



Mwenyezi Mungu anasema:

“(Na akasema Mtume (akilalamika juu ya kufuru ya qaumu yake); Ewe Mola wangu! bila shaka kuwa qaumu yangu wameihama hii qur-ani.”

Suratul-Furqaan,aya - 30



Maelezo ya aya:

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alimshtakia Mola wake kwa (inadi) ya Makafiri wa Kikuraishi kwa kumpinga na kumpigia mifano ya kila aina. Mara wakimwita Mchawi, Mrogaji, Mwendawazimu, Mshairi n.k, na baada ya kukithiri hayo ndio alirejea kwa Mola wake kumshtakia, (na hatukumuona kuelekea kwa (Kofi Annaan, wala kwa Bush wala kwa Wamarekani walanifu wakubwa maadui wa Kiislamu), na katika aliyoshitaki pamoja na kutokutekelezwa yaliyomo katika maamrisho na makatazo, na pia kuihama kwa kuisoma qur-an!na hii shakwa inahusisha hii qaumu yetu ya kiislamu leo, ni wachache ambao alau wanakumbuka kusoma maneno ya Mola wao wote wameshughulika kutafuta haki zao za kisiasa na mihangaiko ya kidunia yalioambatana na maaasi, bali hufunga misafari ili kwenda kupotosha zaidi waja wa Mungu. Na badala ya kuingia katika miji ya kikafiri na kwenda kuwaelimisha na kuwaongoza katika njia ya istigama, wao ndio wa mwanzo kutoa pesa zao katika maasi na kwenda kuyasherehekea, lau pesa hiyo angaliitolea katika njia ya Mungu ikamfutia madhambi,

Eeh! jamani haki ipo kwa Mwenyezi Mungu.



Leo sikumsikia hata mwanasiasa mmoja kutamka kuwa maadili ya

nchini yamekwenda mrama, lakini tumekuwa tayari kuwapeleka watu katika nchi za kikafir ili wausahau Uislamu, na mengi mingi ambayo hata mengine hayafai kutajwa humu ambayo wanayafanya vijana Wakiislamu wa katika nchi za kikafir, yakiwemo wake kwa waume kuoana na wakristo, kuuza miili yao, kunywa mivinyo, kuvuta mabangi, maherwiin (unga wa cocain) na mengi mengine ambayo yanafuta itikadi na imani ya maadili yao ya Kiislamu.

Kwa hivyo wakubwa zetu msituuze huko!!!!!!!!!!!!!!!.ni wajibu wa kila mtu kuwatanabahisha ndugu zetu wa kiisilamu waliopo uhamishoni katika nchi za kikafiri, juu ya kwenda mrama na mafunzo ya kiisilamu na kuwazindua juu ya mbinu za makafiri za kuwapa hifadhi za kisiasa kwani hawatawacha kujaribu kuwapoteza na kuwatoa katika maadili ya kiisilamu kwa kuwahadaisha kwa anasa za kidunia na kuwabakiza Uisilamu jina bila vitendo.



3. Si haya tu, bali wengi hawaridhiki na nywele zao bali hununua za kubandika.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema:

“Amewalani Mwenyezi Mungu wale wanawake ambao wanaunga nywele zao, na wenye kuwaunga……..”



Hadithi hii inatahadharisha wanawake kutenda hayo ili wasije kosa rehema ya Mwenyezi Mungu. Sasa ikiwa hatuna wivu na ndugu zetu wa Kiislamu wa kike basi yanayotufika hii leo katika misuko suko ya huko nyumbani, mojawapo ni kuwapo viongozi wa dini, lakini hawatimizi wajibu wakutoa maadili ya Kisilamu, watu wameshughulishwa na dunia na siasa tu. Ukimuuliza sharti za sala hajui!, bali hata kutawadha mtu utamkuta anavurumisha tu! hatawadhi sawa sawa.



Sasa ikiwa hali imefikia hivi, basi natusubiri naqama itakayotufika, na yaliyo pita ni zinduo kwa Mwenyezi Mungu jee tutazinduka?



4. Na jambo ambalo ni la kustaajabisha zaidi katika hadithi hii tukufu ni kule kuwekwa pamoja mambo mawili haya ya udhalimu wa kisiasa na uchache wa adabu, kwani mambo haya siku zote yanakuwapo pamoja.



Utaona Madhalimu mara nyingi wanawashughulisha watu wao kwa mambo ya starehe na anasa nyingi, na matamanio ya kibinafsi ili wasahau na kupuuza mambo muhimu yenye maslaha kwa watu wote, kama vile kuhimiza kilimo, elimu bora, afya n.k.



Na turejee kwa Mola wetu na kumuomba huku tukimshtakia kwa hii misuko suko ya dunia inayotufika, kwani yeye ndiye mtarajiwa kwa kila kitu, na pia turejeeni katika kitabu chake ambacho kinatupa kila kitu katika mema, na katika kujikanya na mabaya. Kinyume ya hayo ni sawa na kutia maji ndani ya pakacha.



Ewe Mola tushushie rehema yako kwani sisi waja wako tumejidhulumu kwa kutenda makosa mengi,(Ameen).



Wahenga wanasema:

(Usipoziba ufa utajenga ukuta)



Basi na tuwe tayari kuujenga huo ukuta uliovunjika, na kila mmoja

mkubwa na mdogo washike mpini wa kijengeo.



Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema;

“Kila mmoja ni mchungaji, na kila mmoja ataulizwa kwa anachokichunga.”

Hadith Sahih



WABILLAHI TTAUFIIQ

No comments:

Post a Comment