بسم الله الرحمن الرحيم


بسم الله الرحمن الرحيم

UDOMSA.

Wednesday 15 September 2010

QURANI TUKUFU

DARAJA YAKE MBELE YA VITABU VILIVYOTANGULIA
MwenyeziMungu anasema:-
"Na tumekuteremshia kitabu kwa ajili ya kubainisha haki kinachosadikisha vitabu vilivyokuwa kabla yake na kuvihukumia(Wa Muhayminan) kama haya ndiyo yaliyoharibiwa au ndiyo yaliyosalimika".
(Al - Maidah -48).
Na akasema:-
"Na haiwezekani kuwa hii Qurani imetungwa haitoki kwa MwenyeziMungu (kama mnavyodai). Bali imetokana na MwenyeziMungu inayasadikisha yaliyo mbele yake na ni maelezo ya vitabu (vilivyopita) Haina shaka kuwa imetokana kwa Mola wa walimwengu (wote)".
Yunus - 37)
Neno "Wa muhaiyminan" na maana yake ni "Kuvihukumia", na maana yake ni kuwa Qurani imepewa jukumu la kutoa hukmu juu ya vitabu vilivyokuja kabla yake. Na neno “Kuvisadikisha”, maana yake ni kusadikisha yaliyomo, yale ya kweli na kukanusha yaliyoongezwa, yaliyobadilishwa au kugeuzwa pamoja na kuyaamulia kufutwa na pia  kuyathibitisha yaliyo sahihi.
Haya ndiyo anayotakiwa kufuata kila anayeshikamana na vitabu vilivyotangulia, yule ambaye hataki kurudi nyuma akawa kafiri.
Kama alivyosema MwenyeziMungu:-
"Wale tuliowapa kitabu kabla ya hii (Qurani‎) baadhi yao wanaiamini hii (Qurani) na wanaposomewa husema; ‘tunaiamini bila ya shaka hii ni haki itokayo kwa Mola wetu; kwa yakini kabla ya haya tulikuwa wenye kujisalimisha (kwa MwenyeziMungu).”
(Al - Qasas -52)
 
UMMA WOTE UNAWAJIBIKA KUKIFUATA
Watu wote wanawajibika kukifuata kitabu hiki kwa dhahiri na kwa siri na kushikamana nacho na kukisimamia kama ipasavyo.
MwenyeziMungu anasema:-
“Na hii (Qurani) ni kitabu tulichokiteremsha (kwenu) kilicho na baraka nyingi basi kifuateni na muwe wacha Mungu ili Mrehemiwe".
(Al - An - Am - 155)
Na akasema:-
"Fuateni mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu wala msifuate (hao mnaowaitakidi) kuwa walinzi badala yake".
(Al - Aaraf -3)
Na pia akasema:-
"Na wale wanaokishika kitabu (cha MwenyeziMungu kweli kweli) na wakasimamisha Sala (tutawalipa mema) Hakika sisi hatupotezi malipo ya wafanyao mema.”
(Al - Aaraf -170)
Aya zinazoelezea haya ni nyingi, na Mtume (SAW) ameusia juu ya kushikamana na kitabu cha MwenyeziMungu akasema:-
<<Kikamateni kitabu cha MwenyeziMungu na mshikamane nacho>>.
Na katika hadithi iliyoelezwa na Sayiduna Ali(RA) aliyoinyanyua kwa Mtume(SAW), alisema kuwa Mtume (SAW) alisema:-
“Zitakuwa fitina nyingi”.
Nikasema:
“Tufanye nini ili tuepukane nazo ewe Mtume wa MwenyeziMungu?”
Akasema:
“Kitabu cha MwenyeziMungu”.
(Imetolewa na Attirmidhy).
 
KUSHIKAMANA NACHO NA KUKISIMAMIA KAMA KINAVYOSTAHIKI
Uislamu umeshurutisha wafuasi wake kukihifadhi, kukisoma na kukisimamia vilivyo kitabu hiki (Qurani tukufu) usiku na mchana. Kuzizingatia aya zake, kuhalalisha yale yaliyohalalisha kitabu hiki, kuharamisha yaliyoharamisha pamoja  na kuzifuata amri zake, kujiepusha na makatazo yake, kujifunza kutokana na mifano yake, kuwaidhika na visa vyake, kuzifuata vilivyo aya zake zile zilizo wazi maana yake na kusalimu amri juu ya zile zinazotatanisha maana yake (kwa kujiepusha na kuzifasiri kwa matamanio yetu), kutoivuka mipaka yake, kukilinda kutokana na wabadilishaji na waongezaji (wazidishaji mambo yasiyokuwemo ndani yake) walaghai waongo, na kunasihi kutokana nacho kama ipasavyo na kuilingania kwa ujuzi wa kweli.
 
WAADI WA MWENYEZIMUNGU WA KUIHIFADHI(Qurani).
MwenyeziMungu amekwishadhamini kuihifadhi Qurani isifikiwe na mikono ya uongezaji na upunguzaji na ubadilishaji.
MwenyeziMungu anasema:-
"Hakika sisi ndio tulioteremsha mauidha haya (Qurani); na hakika sisi ndio tutakayoyalinda".
(Hijr- 9)
MwenyeziMungu ametaka iwe hivyo ili kuidumisha hoja yake kwa watu na kuifanikisha mpaka hapo atakapoirithi ardhi pamoja vilivyo juu yake (siku ya Kama).
Na hoja hiyo haitoweza kudumu isipokuwa kwa kuendelea kuwepo kwa Qurani hii baina ya watu, huku ikiwa imehifadhika mpaka siku ya Kiama na ili iwe marejeo yao katika mambo ya Itikadi zao za Dini, Misingi yake, Chimbuko lake, Lengo lake na ili tuweze kuzijuwa Sheria za MwenyeziMungu na kubainika kwa wajibu wa yale yanayobainisha(Qurani) na maharamisho yanayokataza na ili kuzijuwa fadhila za kibinadamu pamoja na ukamilifu wa tabia inayofundisha kitabu hiki na kuyaamrisha katika hayo pamoja na kufaidika kutokana na yaliyomo ndani yake katika mongozo ya sheria na kwa kila lililo muhimu katika maisha ya wanadamu.
Tunatakiwa pia kuyasoma mawaidha yake (Qurani), nasaha zake, mifano yake, na mafudisho yake pamoja na yote yaliyomo yenye bishara njema, maonyo, makemeo na njia zote za mafunzo ya malezi ya kila namna inayotuongoza kuelekea njia iliyonyooka.
 USHAHIDI WA KUHIFADHIKA KWAKE.
Inampasa kila mwenye akili timamu aamini na awe na uhakika kuwa Qurani anayoisoma leo, ndiyo ile ile aliyoteremshiwa Muhammad(SAW), na iwapo mtu atachukua aya yoyote ile katika aya za Qurani akaenda nayo London, Paris, Moscow, Washington, Peking au Tel aviv na akatembea nayo katika miji ya Afrika, Australia kisha akenda Makka au Madina au akachukua msahafu kutoka kila mji miongoni mwa miji hiyo na akafungua sura ambazo aya hizo zimetolewa, atagundua kwamba Qurani zote ni moja, na kwamba aya alizozitoa ndani yake ni moja, bali atagundua kwamba kila kilicho ndani ya msahafu wowote ule ni maneno yale yale, hayakugeuzwa wala kubadilika.
MwenyeziMungu amesadikisha aliposema:-
"Hakika sisi ndio tulioteremsha mawaidha haya (hii Qurani) na hakika sisi ndio tutakayoyalinda".
(Al - Hijri 9)
http://www.mawaidha.info/qurani.htm

No comments:

Post a Comment